` TUWEKEZE KATIKA MALEZI YA WATOTO: DKT. JINGU

TUWEKEZE KATIKA MALEZI YA WATOTO: DKT. JINGU

   

Na WMJJWM-Dar es Salaam 

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, amewataka wadau wanaoendesha Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, Makao ya Watoto na Nyumba Salama nchini kuwekeza katika malezi ya Watoto kupitia huduma wanazotoa.


Dkt. Jingu ameyasema hayo Agosti 29, 2025 wakati akizungumza kwenye Kongamano lililowakutanisha Umoja wa Wamiliki wa Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana, Makao ya Watoto na Nyumba Salama ikiwa ni sehemu ya Wiki ya Ustawi wa Jamii katika Viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama Dar Es Salaam.

Amewataka wamiliki hao kuzingatia Sheria, taratibu na Kanuni za uendeshaji wa Vituo hivyo huku akisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya uzalendo kwa watoto ili kujenga Jamii yenye ari na kuipenda nchi yao.

"Tuendelee kushirikiana na kuhakikisha huduma tunazozitoa zinazingatia ubora ili kuwajengea watoto katika misingi bora" amesema Dkt. Jingu.

Amesisitiza kuitambua kazi yao ya utoaji wa huduma ya kijamii na kuimarisha ushirikiano na Serikali kwani inalenga kujenga taifa yenye ustawi wa watoto, kuweka mifumo bora ya utoaji wa taarifa za matukio na vitendo vya ukatili vinavyojitokeza katika vituo.

Aidha, amewahimiza wamiliki hao  kuwaajiri wataalamu wenye sifa na taaluma za  malezi ya watoto na ustawi wa jamii ili kuongeza ubora wa huduma na kuimarisha umoja wenu kitaifa na kikanda.

Dkt. Jingu amesema Serikali katika kuendelea kutekeleza miongozo mbalimbali kuhusu Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa Mwaka wa fedha 2025/26 itawezesha ujenzi wa Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana 154, nyumba Salama 10, Vituo 10 vya Msaada wa Kisaikolojia na huduma nyingine mbalimbali za kiustawi.

Dkt. Jingu amesema Serikali kupitia wadau mbalimbali wa Taasisi za kifedha itashindikana katika kuweka mikakati kwa kushirikiana na Wamiliki hao ili kuwa na mkakati wa kuwa na uendelevu wa Vituo hivyo kujiendesha kwa kupata mikopo kutoka Taasisi za kifedha.

Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Zainab Kitembe, amesema Ofisi hiyo itaendelea kusimamia utoaji wa huduma bora katika Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana, Makao ya Watoto na Nyumba Salama ili watoto waliopo katika maeneo hayo waweze kupata huduma stahiki kwa Ustawi wao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Children in Crossfire (CIC) Craig Fera amesema huduma za ustawi wa Jamii ni muhimu sana katika jamii hasa katika hatua za mwanzo za binadamu za ukuaji wa watoto hivyo sekta ya Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana ni Msingi katika Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Mwakilishi wa UNICEF Mbelwa Gabagambi amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali na Wadau mbalimbali katika kuhakikisha huduma Bora kwa watoto kwenye Vituo vya Kulelea Watoto mchana, Makao ya Watoto na Nyumba Salama zinatolewa kwa kuzingatia miongozo ya Serikali.

Nao umoja wa Wamiliki wa Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana na Makao ya Watoto wamesema wameshirikiana na Serikali na Wadau mbalimbali katika kutoa huduma kwa watoto hasa Malezi na huduma mbalimbali, utoaji wa mafunzo kwa Wataalam wa Malezi kwa watoto na Ustawi wa Jamii ili kuweka kutoa huduma bora zinazozitingatia miongozo na Kanuni zilizopo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464