.jpeg)
Na Neema Sawaka,
JAMII imetakiwa kuendelea kujitoa katika uchangiaji damu ili kuokoa maisha ya wajawazito na watoto wachanga ikiwa ni pamoja na majeruhi wanaopata ajali mbalimbali .
Kundi hilo ndio wamekuwa wahanga katika jamii na wakipata msaada huo wanaweza kupunguza wimbi la kupoteza maisha kutokana na upungufu wa damu.
Akizungumza kwenye zoezi la uchangiaji damu uliofanywa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igunda, iliyopo katika Halmashauri ya Ushetu wilayani hapa, Mganga Mkuu Athumani Matindo, amesema kwa mwezi uhitaji wa damu ni unit 2000 ambapo kwa wiki ni unit 50.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Igunda, Zacharia Ngussa, amesema jamii inatakiwa kuelimishwa juu ya uchangiaji damu ili kuondokana na fikra potofu za kuogopa kushiriki kwenye zoezi hilo.
Mkuu huyo alisema uchangiaji damu kwa jamii inayoishi pembezoni unakuwa wa kusua sua kutokana na kuwepo tafsiri potofu kuwa damu hiyo haiwafikii walengwa bali inauzwa.

Amesema Kama Elimu ikitolewa kwa jamii na ikatambua damu hiyo ni kwa ajili ya wahitaji ambao ni wajawazito , watoto wachanga pamoja na majeruhi itakuwa ni vigumu kuiuza na wengi watajitokeza kuchangia.
Nae Mtekenolojia wa Maabara kutoka Kituo Cha Afya cha Ukune katika Halmashauri ya Ushetu, Afidhi Ally, amesema katika Kituo chake mahitaji ya damu ni makubwa hivyo jamii inatakiwa kuhamasishwa kila mara kuchangia.
Amesema katika Kituo hicho mahitaji ya damu ni unit 20, ambayo kwa asilimia kubwa matumizi yake yamelenga kwa wanawake wajawazito, watoto wachanga na majeruhi pindi yanapojitokeza .


