Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wa Kata ya Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wameeleza kilio chao kuhusu ajali za mara kwa mara zinazotokea katika barabara ya Tinde–Itwangi na kuiomba serikali kuweka matuta ili kudhibiti mwendokasi kwa madereva.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amefanya ziara hiyo jana,ambapo wananchi walieleza kero zao.
Wananchi hao wamesema, katika barabara hiyo kumekuwa na ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu.
“Hii barabara inamaliza watu wetu hasa wanafunzi kumekithiri kwa ajali ni nyingi, madereva wanaendesha kwa kasi sana. vivukio vipo lakini hawafuati sheria za barabarani. Tunaomba serikali itusaidie,” amesema Butu Nkinga.
Naye Kapela Msafiri ameiomba serikali kuweka matuta kwenye barabara hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Itwangi, Kisendi Lubinza, amesisistiza kuwa ajali zimekuwa tishio kubwa kwa usalama wa wananchi na kuomba serikali ichukue hatua za haraka.
“Wananchi wamezungumza mengi, lakini napenda kusisitiza kuhusu ajali hizi. Tunaomba serikali iweke matuta, jamani tutaisha kwenye hii barabara,” amesema Lubinza.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema serikali inalifahamu tatizo hilo na tayari imeanza kulifanyia kazi kwa kushirikiana na kamati husika.
Pamoja na mambo mengine Mkuu huyo wa wilaya, amesema kero zao zote ambazo wameziwasilisha kwake zitafanyiwa kazi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464