` MWANAMKE PENDO ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUMUUA MPENZI WAKE KWA WEMBE NYUMBA YA KULALA WAGENI

MWANAMKE PENDO ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUMUUA MPENZI WAKE KWA WEMBE NYUMBA YA KULALA WAGENI

Mwanamke Pendo ashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake kwa wembe

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MWANAMKE aitwaye Pendo Samson Medusela (37), mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Timithoy Magesa (35), kwa kumkata kwa wembe sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na wivu wa kimapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amebainisha hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, na kueleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 23 mwaka huu, majira ya saa 3 usiku, katika nyumba ya wageni ya Bwashee, iliyopo Ndala Manispaa ya Shinyanga.

Amesema kabla ya mauaji hayo, Pendo alipigiwa simu na mwanamke mwingine kwa kutumia simu ya marehemu, akimuonya aachane naye kwa madai kwamba ndiye anayempenda. baada ya muda Timothy alimtafuta Pendo na kumtaka wakutane katika nyumba ya wageni hiyo ili wazungumze.

“Hata hivyo, walipokutana walianza kugombana kuhusu mwanamke aliyempigia simu, hali iliyosababisha Pendo kutumia wembe aliokuwa nao kumkata Timothy sehemu mbalimbali za mwili na kuvuja damu nyingi,” amesema Kamanda Magomi.

Ameongeza kuwa, marehemu alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda Magomi amesema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi na kueleza kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha, amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi na badala yake kutumia njia za amani kutafuta suluhu pindi wanapokumbwa na migogoro ya kimahusiano.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464