` TCRA:VYOMBO VYA HABARI VYA MTANDAONI MSIANDIKE HABARI ZA UVUMI KIPINDI CHA UCHAGUZI

TCRA:VYOMBO VYA HABARI VYA MTANDAONI MSIANDIKE HABARI ZA UVUMI KIPINDI CHA UCHAGUZI

Na Marco Maduhu,MWANZA

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)imevitaka vyombo vya habari mtandaoni kuepuka kuandika habari za uvumi kipindi cha uchaguzi mkuu 2025.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 7,2025 na Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)Mhandisi Andrew Kisaka, wakati akiwasilisha mada kwenye semina ya waandishi wa habari Kanda ya Ziwa na Jeshi la Polisi kuelekea uchaguzi Mkuu 2025.

Amesema vyombo vya mtandaoni vinapaswa kuwa makini katika kuripoti habari za uchaguzi 2025 na kuacha kuandika habari za uvumi,bali waandike habari sahihi, ili kuepuka kupotosha umma na kuleta taharuki.

"Vyombo vya habari vya mtandaoni, wanapenda sana kuandika habari za uvumi ili wapate "viewers"sasa kipindi hiki cha uchaguzi, mnapaswa kuwa makini na kuripoti habari zilizo sahihi," amesema Mhandisi Kisaka.

Amewataka pia waandishi wa habari wa vyombo vyote kwa katika kipindi hicho cha uchaguzi wasiandike habari au kutangaza maoni yao binafsi pamoja na kuhariri habari kwa usahihi.

Amewasisitiza pia katika uchaguzi huo, watangaze sera za uchaguzi za vyama vya siasa,kwa kuwauliza wagombea nini watakifanya kwa wananchi kupitia sera za vyama vyao.

Aidha,katika Semina hiyo Mhadisi Andrew Kisaka,amewasilisha Mada ya"Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya siasa za mwaka 2020 ambazo pia zitatumika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464