` ASCENDING AFRICA YAZINDUA MRADI WA JAHAZI, KUIMARISHA DHAMIRA YA KULINDA UCHUMI WA BULUU AFRIKA MASHARIKI

ASCENDING AFRICA YAZINDUA MRADI WA JAHAZI, KUIMARISHA DHAMIRA YA KULINDA UCHUMI WA BULUU AFRIKA MASHARIKI


Leo Agosti 19, 2025, Ascending Africa imetangaza mabadiliko ya mradi wake mkuu wa uhifadhi wa bahari kutoka kuitwa Kilindini kuwa Mradi wa Jahazi; hatua inayolenga kupanua wigo, kuongeza nguvu mpya na kuimarisha dhamira ya kulinda Pwani ya Afrika Mashariki na ya mataifa yaliyopo Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi. 

Hatua hii inakuja wakati ambapo Uchumi wa Buluu wa ukanda wa Afrika Mashariki unaotarajiwa kufikia Dola za Kimarekani bilioni 405 ifikapo mwaka 2030, unakabiliwa na vitisho vikubwa kutokana na uwepo wa uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa.

 Aina hii ya uvuvi inazisababishia nchi za Afrika ya Mashariki hasara ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 415 kila mwaka, pamoja na kupunguza kwa kasi kubwa akiba ya samaki ambayo mamilioni ya watu hutegemea kwa usalama wa chakula na kipato.

Jahazi,” ni neno la Kiswahili linalomaanisha chombo cha jadi cha kusafiria baharini, linaakisi urithi wa kihistoria na wa kitamaduni wa bahari katika Pwani ya Afrika Mashariki na linatumika kama taswira ya mabadiliko kwa jamii za Pwani katika kuelekea ustawi endelevu wa Bahari.

“Uchumi wa Buluu una nafasi kubwa mno kwa Afrika Mashariki, lakini ahadi hii ipo hatarini. Uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa pamoja na mbinu za uvuvi zisizo endelevu zinatishia bahari yetu na riziki za mamilioni ya watu wanaoitegemea,” alisema Michael Mallya, Msemaji wa Mradi wa Jahazi.

“Serikali na wadau wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii kufanya usimamizi, udhibiti na uwezeshaji wa jamii za mwambao wa pwani. Kupitia Mradi wa Jahazi, tumejipanga kuungana nao, kuongeza nguvu katika juhudi hizo na kuhakikisha bahari zetu zinabaki zenye uwingi wa rasilimali kwa vizazi vijavyo.” aliongeza Mallya.

Mradi wa Jahazi utashirikiana na serikali za Afrika Mashariki, wawekezaji wa ndani, asasi zisizo za kiserikali (NGOs), na viongozi wa jamii husika ili kupambana na Uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa (IUUF), kulinda mifumo ya ikolojia ya bahari na kukuza uchumi shirikishi na endelevu. Juhudi hizi zitahusisha utetezi wa sera za kulinda bahari, ushirikiano katika kuimarisha usalama wa bahari, uhifadhi unaosimamiwa na jamii nzima, pamoja na kampeni za elimu ili kuhamasisha njia za uvuvi endelevu.

Kuhusu Mradi wa Jahazi

Mradi wa Jahazi, unaoongozwa na Ascending Africa, ni mpango wa kikanda unaolenga kufufua Uchumi wa Buluu wa Afrika Mashariki huku ukihakikisha uendelevu wa muda mrefu wa rasilimali za baharini. Ukiwa na picha ya alama ya kitamaduni ya jahazi, mradi huu unaunganisha urithi, usimamizi wa mazingira na fursa za kiuchumi katika harakati za kujenga Pwani yenye ustawi na uimara. Kiini cha jitihada hizi ni mapambano dhidi ya uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa (IUUF) ambao unatishia kukatisha riziki za jamii za watu wa Pwani na kudhoofisha maendeleo endelevu katika ukanda mzima.

Kuhusu Ascending Africa

Ascending Africa ni Shirika la ki-Afrika lililojitolea kukuza maendeleo endelevu barani kote, likizingatia uhifadhi wa mazingira, mikakati ya uwezeshaji wa jamii na ukuaji wa kiuchumi.

Kwa maelezo zaidi kuhusu mikakati hii, tembelea tovuti za Mradi wa Jahazi na Ascending Africahttps://jahaziproject.org

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464