
Leo Julai 2,2025 Bw. Hilali Alexander Ruhundwa amerejesha fomu ya kuwania ubunge jimbo la Ngara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ruhundwa ambaye ni mwandishi wa habari mwandamizi na mhariri mkuu wa jukwaa la redio za jamii Tanzania radiotadio.co.tz amekuwa miongoni mwa makada wanaoomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi kupeperusha bendera katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu.
Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kufahamu vipaumbele vyake endapo ataaminiwa na CCM kuwakilisha wananchi wa Ngara, Ruhundwa ameeleza kuwa yeye ni muumini wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu hivyo atahakikisha kuwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inatumika kwa kiasi kikubwa katika kila nyanja ndani ya jimbo la Ngara.
Elimu: Ruhundwa anaamini kuwa dunia imebadilika na kwa sasa teknolojia ni kila kitu. Anasema atahakikisha kuwa kila shule ya sekondari ndani ya Ngara inakuwa na vifaa vya kutosha sanjari na wataalam wa Tehama lengo ni kuhakikisha kuwa Ngara inazalisha wahitimu wengi wenye ujuzi wa teknolojia watakaoleta ushindani katika soko la ajira la dunia.
Kadhalika Ruhundwa anasema atavishawishi vyuo vikuu nchini na nje ya nchi hasa vya nchi jirani kujenga matawi ya vyuo hivyo ndani ya Ngara. Hili lilikuwa kwenye ilani yake wakati anatia nia ya ubunge mwaka 2020 na mpaka sasa anaamini kuwa uwepo wa vyuo hivyo ndani ya Ngara utaongeza wigo wa elimu, ajira na biashara ndani ya Ngara.
Kuwashauri wanafunzi kujikita kwenye elimu yenye soko duniani. Maendeleo ya teknolojia duniani yanahitaji wajuzi wa teknolojia zaidi hivyo Ruhundwa atahakikisha kuwa wanafunzi wanajikita kupata elimu itakayowasaidia kupata ajira popote duniani.
Ruhundwa anasema atahakikisha kuwa kuna vituo vikubwa viwili vya Tehama ndani ya Ngara ili kuwapa fursa vijana wabunifu na wananchi kwa ujumla kupata maarifa ya teknolojia na kutumia fursa za teknolojia zilizopo duniani pote.
Viwanda: Ruhundwa anasema atatumia ushawishi alionao ndani na nje ya nchi kuleta wawekezaji kujenda viwanda ndani ya Ngara. Anaamini kuwa baada ya nchi za Magharibi kukata misaada kwa nchi za Afrika hasa kwenye sekta ya Afya, mahitaji ya vifaa tiba ni makubwa hivyo nchi itategemea viwanda vya ndani hivyo ni fursa kubwa kwa wakai wa Ngara kuneemeka kwa viwanda hivyo.
Kuhusu Kilimo: Ruhundwa anasema atahakikisha analeta wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kupima afya ya udongo na kubaini mazao ya biashara na chakula yanayofaa kulimwa. Kwa kutumia bioteknolojia wananchi wa Ngara watazalisha mazao kwa wingi na kuongeza kipato.
Vilevile Ruhundwa anasisitiza kuwa ataleta wawekezaji kuwekeza kwenye sekta ya kilimo kwa kuanzisha mazao mapya ya biashara na kujenga viwanda vya kuchakata mazao hayo na kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Ufugaji: Ruhundwa anasema atahakikisha analeta wataalam wa mifugo watakaowajengea uwezo wafugaji namna ya kufuga kisasa kwa kutumia teknolojia na kuongeza idadi ya wanyama. Hili litaenda sambamba na kuanzisha kiwanda cha kuzalisha bidhaa zitokanazo na mifugo kama ngozi kutengeneza viatu, mikoba, mikanda nk.
Uanzishwaji wa Bandari ya nchi Kavu: Ruhundwa anasema jiografia ya Ngara inaiwezesha kuwa na bandari ya nchi kavu hivyo atahakikisha anaishauri serikali na sekta binafsi kujenga bandari hiyo itakayohudumia nchi jirani tofauti na sasa wafanyabishara wa nchi hizo wanavyosafiri umbali mrefu kwenda bandari ya Dar es Salaam.
Ushirikiano wa Sekta Binafsi na Serikali: Ruhundwa anaamini kuwa sekta binafsi ni nguzo kuu ya maendeleo hivyo atahakikisha anaishauri serikali kutumia sekta na watu binafsi kutoa huduma kama maji ndani ya Ngara. Kwa kufanya hivi huduma zitawafikia wananchi kwa haraka na kwa ubora huku serikali ikihusika na ushuru.
Kuhusu Michezo: Ruhundwa anasema Ngara imebarikiwa kuwa na vipaji vingi hasa kwenye michezo hivyo atahakikisha kuwa Ngara inakuwa na timu za wanaume na wanawake wanaoiwakilisha Ngara kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Utamaduni: Ruhundwa anaamini kuwa utamaduni ni nyenzo kuu ya maendeleo ya jamii na taifa. Ataanzisha kituo cha makumbusho ya utamaduni wa wakazi wa Ngara ikiwa ni pamoja na kuwa na ngoma za asili zitakazorekodiwa na kuhifadhiwa kwa njia ya teknolojia kuitangaza Ngara kitaifa na kimataifa. Hii pia itaondoa usumbufu kwa wazaliwa wa Ngara kusumbuliwa na Idara ya Uhamiaji kuhusu uraia.
Kuwa na Baraza la Wazee Ngara lenye nguvu: Ruhundwa anaamini kuwa wazee ni hazina kubwa katika jamii kwani wameona ya zamani, ya sasa na wanaweza kubashiri yajayo. Baraza hili litakuwa lenye heshima Ngara ambalo litashauri viongozi kwa kupendekeza vipaumbele vya maendeleo ya Ngara sanjari na kuonya pale viongozi watakapokengeuka.
Kuimarisha mahusiano mema baina ya Wanangara: Ruhundwa atahakikisha anawaunganisha Wanangara na kuwa kitu kimoja. Atahakikisha pia wasomi na wafanyabiashara kutoka Ngara wanakuwa na mazingira mazuri ya kuwekeza nyumbani Ngara.
Ruhundwa ambaye amekuwa akijishughulisha na siasa kwa muda mrefu hasa wakati akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipoanzisha tawi la UVCCM la SJMC-UDSM, amekuwa na ndoto za kuona Ngara inakuwa kitovu cha uchumi kwa Kanda ya Ziwa kutokana na jiografia yake kupakana na nchi nyingi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464