TRILIONI 1.5 ZAIMARISHA ELIMU, AFYA, MAJI NA MIUNDOMBINU SHINYANGA
TRILIONI 1.5 ZAIMARISHA ELIMU, AFYA, MAJI NA MIUNDOMBINU SHINYANGA
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mkoa wa Shinyanga umepokea zaidi ya shilingi trilioni 1.56 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ambapo Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 150.26 zilikusanywa kama mapato ya ndani ya Halmashauri, sawa na asilimia 98 ya lengo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mohamed Mhita ameeleza hayo leo July 14,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa takwimu hizo ni ushahidi wa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo yanayoonekana na kugusa maisha yao moja kwa moja.
Katika sekta ya elimu pekee, amesema Mkoa umepokea shilingi bilioni 155.24, zilizowezesha ujenzi wa shule mpya, mabweni, maktaba, maabara na vyuo. Idadi ya shule za sekondari imeongezeka kutoka 186 hadi 200, na vyumba vya madarasa ya sekondari vimeongezeka kutoka 1,583 hadi 2,865.
Kwa Upande wa afya amesema Sekta hiyo imeimarishwa kwa shilingi bilioni 79.1, ambapo hospitali mpya tano za wilaya zimejengwa, zahanati zimeongezeka kutoka 226 hadi 277, na vituo vya afya kutoka 25 hadi 38. Vilevile, upatikanaji wa dawa umeongezeka kutoka asilimia 76 hadi asilimia 88 mwaka 2025.
Mhita amesema Sekta ya maji pia imepokea shilingi bilioni 113.33, ambazo zimewezesha vijiji vyenye huduma ya maji kuongezeka kutoka 162 hadi 384. Miradi mikubwa kama ule wa maji kutoka Ziwa Victoria umeendelea kutekelezwa katika maeneo ya Kahama, Kishapu na Ushetu.
Katika mapato yatokanayo na madini,amefafanua kuwa Mkoa wa Shinyanga umekusanya shilingi bilioni 540.17 kwa miaka minne, na mapato ya Halmashauri kutokana na sekta hiyo yamepanda kutoka milioni 745 hadi zaidi ya bilioni 3.3. Wachimbaji wadogo waliopewa leseni wameongezeka kutoka 332 hadi 1,766.
Kwa Upande wa Miundombinu amesema shilingi bilioni 221.19 zilitumika kujenga barabara za lami na changarawe, madaraja na makalavati. Mtandao wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 224 hadi 281.
Kwa upande wa umeme, Mkuu huyo wa Mkoa wa Shinyanga amesema vijiji vyote 506 vya mkoa huo sasa vimeunganishwa na umeme, huku miradi 133 ya usambazaji ikiendelea. Shirika la TANESCO limetumia bilioni 492 kufanikisha kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na kugawa mitungi 6,500 ya gesi kwa ajili ya nishati safi ya kupikia.
Amesema Mkoa pia umefanikiwa kupima viwanja 10,658 kwa ajili ya biashara, huduma na uwekezaji – huku maeneo kama Chapulwa, Zongomela, Ibadakuli na Nyashimbi yakitengwa rasmi kwa uwekezaji wa viwanda.