INEC:WANAO OMBA KUPIGA KURA MOJA YA RAIS NJE YA VITUO WALIVYOJIANDIKISHA UCHAGUZI MKUU 2025 WAHUDUMIWE
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, amewakumbusha watendaji wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 kuzingatia mafunzo waliyopewa,ikiwamo kuwahudumia wapiga kura wanaoomba kupiga kura moja ya Rais nje ya vituo walivyojiandikisha.
Jaji Mwambegele ametoa kauli hiyo leo Julai 23, wakati akihitimisha mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa uchaguzi wa ngazi ya majimbo kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu, yaliyofanyika mkoani Shinyanga kuanzia Julai 21.
Amesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu baadhi ya sheria zimebadilika, ikiwamo ya wapiga kura kuomba kupiga kura moja ya Rais nje ya vituo walivyojiandikisha, na namna ya kusimamia uchaguzi kwenye maeneo yenye mgombea mmoja, na jinsi ya kusimamia kura zitakazopigwa magereza.
“Natumaini yangu kwamba maeneo mapya mliyojifunza mmeyaelewa vizuri,mfano namna ya kuwahudumia wapiga kura wanaoomba kupiga kura moja ya Rais nje ya vituo walivyojiandikisha, kusimamia uchaguzi kwenye maeneo ya Mgombea Mmoja,na kusimamia kura zitakazopigwa magereza, haya ni machache ambayo hayakuwapo kwenye sheria zilizopita na hakuna mwenye uzoefu nayo,”amesema Jaji Mwambegele.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji hao wa uchaguzi Mkuu,kwamba katika kipindi hiki wayapuuze makundi ya WhatsApp, ili wasije kukosea kutuma taarifa ya aina yoyote katika makundi hayo ambayo haitakiwi kutumwa huko.
Amesema kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo,walikuwa kiapo cha kutunza siri, na kwamba ukiukaji wa kiapo hicho na kutoa taarifa za siri ambazo Tume haijaelekeza kutolewa,watakuwa wametenda kosa na watawajibishwa kwa kosa hilo, na hivyo kuwataka wawe makini na makundi Sogozi ya WhatsApp.
“sasa kuna makundi sogozi ya WhatsApp niwatahadharishe kipindi hiki myapuuze ili msije kukosea kutuma taarifa ya aina yoyote katika makundi hayo ambayo haikutakiwa kutumwa huko.”amesema Jaji Mwambegele.
Amewasisitiza pia, kubandika mabango yenye orodha ya majina ya wapiga kura na matangazo au taarifa zinazopaswa kuwafikia wapiga kura kulingana na kalenda, na isije jitokeza kama ilivyokuwa kwenye zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura, ambapo kulikuwa na changamoto hiyo ya kutobandikwa mabango
Mwenyekiti wa mafunzo hayo Faustine Lwagwen, akizungumza kwa niaba ya wenzake, amesema yale yote ambayo wamefundishwa watakwenda kuyatekeleza ipasavyo pamoja na kuzingatia miongozo,kanuni na maelekezo kutoka Tume.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati ya INEC katika kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru, wa haki, wenye uwazi na unaokubalika na wadau wote, ambayo yametolewa kwa watendaji wa Uchaguzi, ambao ni Waratibu wa uchaguzi,wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi ngazi ya Jimbo.
TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza.
Mafunzo yakiendelea.