` MGEJA AMTAKA POLEPOLE AWAOMBE RADHI WAJUMBE WA MKUTANO MKUU CCM

MGEJA AMTAKA POLEPOLE AWAOMBE RADHI WAJUMBE WA MKUTANO MKUU CCM

MGEJA AMTAKA POLEPOLE AWAOMBE RADHI WAJUMBE WA MKUTANO MKUU CCM

******

SAKATA la kauli ambazao zimeendelea kutolewa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Polepole limeendelea kupamba moto baada ya mmoja wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Khamis Mgeja kumtaka awaombe radhi wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa.

Mgeja ametoa kauli hiyo akiwa anaendelea na matibabu yake nchini India ambapo alisema Polepole alipaswa kuheshimu maamuzi ambayo yalitolewa na Mkutano Mkuu huo maalumu wa CCM uliowapitisha, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Hussein Mwinyi na Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa wagombea kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Alisema yeye binafsi pamoja na kwamba yupo kwenye matibabu nchini India lakini anasikitishwa na kauli za Polepole anazozisikia kupitia mitandao ya kijamii akituhumu na kupinga maamuzi ambayo yalitolewa na mkutano mkuu wa CCM Taifa wa kuwapitisha mapema wagombea wake wa nafasi za urais wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.

“Naomba nimweleze jambo moja ndugu yetu Polepole, pamoja na usomi wake lakini huenda haijui vizuri Katiba ya Chama cha Mapinduzi na hivyo anashindwa kuitafsri kwa usahihi na ndiyo maana hoja zake zote za malalamiko hajawahi kutaja Ibara ama kifungu cha katiba kilichokosewa na wajumbe,”

“Badala yake ameishia kudai desturi na utamaduni haukufuatwa na kuzingatiwa, hii ni wazi ni sawa na ujinga na kutoifahamu vizuri Katiba ya Chama, lakini nimfahamishe Polepole na kundi lake lililojificha kwamba, taratibu zote za uteuzi wa wagombea wa CCM zilifuatwa na zilizingatia matakwa ya Katiba,” alieleza Mgeja.

Aliendelea kueleza kuwa katika kufikia maamuzi hayo, wajumbe wa mkutano mkuu walizingatia matakwa ya Katiba na ikibidi wakasome Ibara ya 102 na ibara ya 101 na vifungu vyake vidogo ndipo watajua uhalali wa maamuzi ya uteuzi wa wagombea Urais na mgombea mwenza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi na mchakato huo ulikuwa wa wazi kabisa.

Mgeja alifafanua kuwa mara baada ya pendekezo la kumteua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wazee wa Chama wakiongozwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete walitoa ushauri wa suala hilo kuletwa rasmi katika mkutano huo kama agenda.

“Tulishuhudia mkutano ukiahirishwa ili kupisha vikao vya Sekretarieti, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ambavyo vilikaa na kisha kupeleka mbele ya mkutano mkuu mapendekezo ya jina moja la mgombea urais kwa tiketi ya CCM kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu wa 2025,”

“Jina lililopendekezwa lilizingatia matakwa ya kanuni inayoeleza kuwa majina yatakayopendekezwa yasizidi matatu, hivyo linaweza kuwa moja, mawili ama matatu, sasa huenda hapa mwenzetu Polepole ndipo alipopigwa chenga, maana yasizidi matatu, lazima ianzie moja ili mradi yasizidi matatu,” alieleza Mgeja.

Mgeja amemuomba Polepole aitishe Meza ya mjadala kwa yote ili aweze kupatiwa majibu na kukumbushwa mambo ya nyuma ya awamu ya tano jinsi gani Chama walivyokigeuza kama Kampuni yao binafsi na kupora mamlaka ya wanachama.

“Awamu hiyo tulishuhudia demokrasia ikikandamizwa, uhuru wa kujieleza ukikandamizwa huku watu wakidhulumiwa fedha zao kwenye akaunti zao ambapo walikuta fedha zimechukuliwa na akaunti zipo tupu huku wakilimbikizwa kodi za hovyo,”

“Tulishuhudia mahusiano yetu na nchi za nje ya kidiplomasia yakipungua kila siku, matumizi mabaya ya fedha za umma kiasi cha kumfukuza kazi CAG aliyefichua uchafu huo, huku watumishi wa umma wakifukuzwa kazi kwa kile kilichodaiwa kutumbua majipu, huku wengine mpaka sasa wakilipwa mishahara pasipo kufanya kazi,” alieleza.

Alisema mambo mengi ya hovyo yalifanyika katika kipindi hicho cha awamu ya tano huku Polepole akiwa mmoja wa washauri wa karibu ndani ya Serikali lakini hakuwahi kukemea wala kupinga vitendo hivyo visifanyike badala yake alidai mji ulikuwa na mwenyewe tofauti na sasa eti mji hauna mwenyewe.

Alisema kauli za Polepole kwa hivi sasa zinawashangaza watu wengi wenye uelewa mpana wa kifikra na kwamba yeye binafsi (Mgeja) anamuomba Polepole ajaribu kuwapa heshima wanayostahili wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa na ajitokeza kuwaomba radhi kwa kauli yake ya kihuni kwamba mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM ulinajisiwa.

“Nimfahamishe wanachama wa CCM wanaoifahamu vizuri Katiba na kanuni za CCM na kwamba iwapo Polepole na kundi lake walikuwa na jina linguine la mgombea wao wa Urais, basi kwa awamu hii imekula kwao na watafute kazi nyingine kwani CCM tayari ina wagombea wake, Dkt. Samia, Dkt. Hussein na Balozi Dkt. Nchimbi,”

“Tunaamini kwa kazi kubwa ambazo zimefanyika ndani ya kipindi hiki cha cha kwanza cha awamu ya sita wagombea wote wa CCM watapata kura za kishindo kwa vile wanabebwa na kazi walizozifanya ambazo kwa sehemu kubwa zimewaletea maendeleo watanzania,” alieleza Mgeja.

Aliendelea kueleza kuwa Tanzania ni nchi ina wenyewe na iko imara na Polepole aache tabia ya kujifananisha na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba anaweza kukemea jambo lolote kwenye nchi hii bali aelewe yeye kisiasa bado ni mwepesi sana mfano wa sufi na hajaota mizizi anaelea kama magugu maji.

Mwisho Mgeja amemshangaa Polepole kuhusiana na suala la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuapiswa kuwa Rais wa Tanzania baada ya kifo cha mtangulizi wake Hayati John Pombe Magufuli na badala yake CCM ingeitisha uchaguzi ndani ya Chama na kufanyike uchaguzi mkuu.

“Kauli hii pia ni upotoshaji ambayo Polepole ameifanya kwa makusudi kutaka kuwapotosha watanzania kwani yeye mwenyewe anafahamu fika matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 37 inayozungumzia suala la Rais aliyepo madarakani kufarini hatua zipi zifanyike kumpata Rais mwingine.

“Kwa haya yote yanayoelezwa na Polepole kwa lengo la kutaka kuupotosha umma wa Watanzania, anastahili kuchukuliwa hatua za kisheria za uchochezi kama zinavyochukuliwa kwa wachochezi wengine na pia Chama kichukue hatua za kimaadili dhidi yake ili iwe mfano kwa wengi wenye lengo la kutaka kuchafu hali ya hewa hapa nchini,” alieleza Mgeja.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464