` MADEREVA WAFUNGIWA LESENI SHINYANGA WAENDESHA MWENDOKASI KILOMITA 118 KWA SAA MFULULIZO

MADEREVA WAFUNGIWA LESENI SHINYANGA WAENDESHA MWENDOKASI KILOMITA 118 KWA SAA MFULULIZO

MADEREVA WAFUNGIWA LESENI SHINYANGA WAENDESHA MWENDOKASI KILOMITA 118 KWA SAA MFULULIZO

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewafungia leseni madereva watatu kwa kipindi cha miezi mitatu kila mmoja, baada ya kubainika kuendesha magari kwa mwendokasi, kati ya kilomita 100 hadi 118 kwa saa mfululizo, kinyume na sheria za usalama barabarani.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi,amebainisha hayo leo Julai 23,2025 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari,kwa kipindi cha kuanzia Juni hadi Julai 22 mwaka huu.
Amesema kwa kipindi hicho kupitia kikosi cha usalama barabarani, wamefanikiwa kukamata makosa ya usalama barabarani 5,759, pamoja na kuwafungia leseni madereva watatu kutokana na kuendesha gari kwa mwendokasi.

“Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha usalama barabarani tumekamata madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani na kukamata makosa 5,759,katika makosa haya magari ni 4,557, na tumefungia leseni zao madereva watatu kwa kipindi cha miezi mitatu kila mmoja,”amesema Magomi.

Amesema, kwa upande wa pikipiki na bajaji wamekamata makosa 1,202 na kwamba madereva wengine waliokamatwa na makosa mbalimbali ya usalama barabarani wakiwamo wa magari waliwajibishwa kwa kulipa faini ya papo kwa hapo.

Aidha, Kamanda Magomi alibainisha kuwa jeshi hilo pia limewakamata watuhumiwa 125 kwa makosa mbalimbali ya uhalifu, wakiwa na vielelezo mbalimbali ikiwemo gramu 2,261 za bangi, lita 142 za pombe ya moshi, kilo 29 za mirungi, pamoja na vifaa vingine ikiwemo bajaji moja, runinga 7, mabati 16, nondo 17, vitanda vinne, redio 8 na pikipiki 22.

Katika hatua nyingine, Jeshi hilo limeendesha mikutano 64 ya kutoa elimu kwa wananchi, wadau na madereva wa vyombo vya moto, ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuhimiza uzingatiaji wa sheria na kanuni za usalama barabarani.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464