MAHAFALI YA 13 CHUO CHA SAYANSI ZA AFYA KOLANDOTO NA MAHAFALI YA PILI TAWI LA MWANZA YAFANA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MAHAFALI ya 13 Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto,na Mahafali ya Pili Tawi la Mwanza yamefana.
Mahafali hayo yamefanyika leo Julai 18,2025 katika Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto,na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wazazi.
Akizungumza katika Mahafali hayo Mgeni Rasmi Makamu Askofu Mkuu Kanisa la AICT Zakayo Enock Bugota,amewataka wahitimu hao wakawe mabalozi wazuri, katika kuzingatia uadilifu ili kukitangaza chuo chao kwa kutoa wanafunzi wenye maadili mema.
Amesema,hana shaka na elimu na ujuzi ambao wamepata Chuoni hapo, sababu ni Chuo chenye kutoa elimu bora na hivyo kuwasihi Wahitimu hao, wakazingatie yale ambayo wamefundishwa pamoja na kuwa uadilifu na kuzingatia miiko ya taaluma yao.
"Jinsi mlivyopendeza leo na huduma zenu zipendeze hivyo hivyo katika kuhudumia Wagonjwa,"amesema Askofu Bugota.
Aidha,amewataka pia Wahitimu hao kwamba kila hatua ambayo wanaifanya wamtangulize Mungu, sababu yeye ndiyo atanyoosha mapito yao na hata kupata Ajira.
Katika hatua nyingine, ameiomba Serikali kuongeza nguvu kutoa mikopo kwa Vyuo vya Kati,ili wanafunzi wa hali ya chini wasishindwe kumaliza masomo yao.
Pia, ameipongeza serikali kwa kutoa fursa ya Chuo hicho,kiwe na hadhi ya Chuo Kikuu pamoja na kuupongeza uongozi wa Chuo kwa kuboresha miundombinu na kuongeza Idadi kubwa ya Udahili wa wanafunzi.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga David Lyamongi, amesema serikali itaendelea kushirikiana na Chuo hicho.
Amesema,serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya Afya, ikiwamo kuboresha miundombinu na kutoa Ajira.
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Paschal Shiluka, amesema Chuo hicho kwa sasa kina uwezo wa kudahili wanafunzi 1,800,kutoka wanafunzi 300 Mwaka 2012.
Ametaja Idadi ya Wahitimu wa Taaluma mbalimbali Chuoni hapo, kwamba wamehitimu wanafunzi 207,huku Tawi lao la Mwanza wamehitimu 36, na kwamba kati ya wanafunzi hao wote, 45 wameshindwa kumaliza masomo yao zikiwamo sababu za ukosefu wa Ada.
Nao baadhi ya Wahitimu hao,wamesema watayazingatia yale ambayo wamefundishwa pamoja na kuwa na maadili mema.
TAZAMA PICHA👇👇
Makamu Askofu Mkuu Kanisa la AICT Zakayo Enock Bugota akizungumza.
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Paschal Shiluka akizungumza.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga David Lyamongi akizungumza.
Dk. Mstaafu Emmanuel Mwandu akizungumza.
Picha za pamoja zikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464