Mtia nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Itwangi Fadhili Nafutari
Na Mwandishi wa Shinyanga Press Club Blog
Fadhili Salmon Nafutari, Mtanzania
mzalendo na kijana mwenye maono ya kweli ya maendeleo, ametangaza rasmi nia
yake ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Itwangi, Wilaya ya Shinyanga
akiwa na msukumo wa kulijenga jimbo hilo kupitia rasilimali zake za asili na
nguvu kazi ya wananchi wake.
Fadhili anakuja na dira mpya ya maendeleo
yenye kugusa maisha ya kila mwananchi,ambapo katika hotuba yake ya kutangaza nia amesema Itwangi
ni miongoni mwa maeneo ya Shinyanga yenye utajiri mkubwa wa rasilimali, hasa
madini na ardhi yenye rutuba, lakini bado fursa hizo hazijawanufaisha kikamilifu.
“Itwangi ina madini wananchi wake
wanahitaji kupimiwa maeneo yao rasmi ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye
shughuli za uchimbaji, kuanzisha vikundi vya uchimbaji wa pamoja, na kupewa
elimu juu ya thamani ya madini wanayoyapata kwa kufanya hivi, tutaondoa
unyonyaji na kuwawezesha wananchi wetu kupata kipato halali na cha kudumu,”
amesema Fadhili.
Mbali na Sekta ya madini, Fadhili
amesema suluhisho la kudumu kwa changamoto ya kilimo ni kuchimba na kuendeleza
marambo ya maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji,kutokana na kuwa na maeneo
mengi yanayofaa kwa uchimbaji wa mabwawa ya maji (marambo) ambayo yakitumika
vyema yatawezesha wakulima kulima kwa msimu wote na kujiongezea kipato.
“Tutachimba marambo ya maji kwa ajili
ya kilimo cha umwagiliaji hili litasaidia wakulima kuondokana na utegemezi wa
mvua na kuongeza uzalishaji hata kipindi cha kiangazi na itaimarisha usalama wa
chakula na kuinua pato la familia nyingi za wakulima,” ameongeza.
Ajenda Kuu za Fadhili Nafutari kwa
Jimbo la Itwangi moja ni kuendeleza Sekta ya Madini kwa kupima maeneo ya
madini, kuwawezesha wachimbaji wadogo, kuanzisha saccos na vikundi vya vijana
na wanawake kwenye sekta hiyo.
Jambo la pili ni kuhakikisha
wananchi wanalima kilimo cha Umwagiliaji kupitia marambo ya maji yatakayochimbwa
na ujenzi wa miundombinu rafiki ya kilimo cha kisasa ili kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi,na tatu ni kuwezesha Vijana na Wanawake Kiuchumi elimu ya ujasiriamali, mikopo ya vikundi na kuunganisha
na taasisi za fedha kwa maendeleo endelevu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464