Madiwani Shydc wapitisha rasimu ya sheria ndogo za halmashauri
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, wamepitisha rasimu ya marekebisho ya sheria ndogo,za Ada na Ushuru za Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Rasimu hiyo imepitishwa leo Juni 18, 2025 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili ajenda moja ya kupitisha mabadiliko hayo
Awali Wakili wa Serikali Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Salehe Hassan,akiwalisha rasimu hiyo,amesema sheria ndogo ambazo wanazirekebisha ni za mwaka 2018,ambazo zimeshapitwa na wakati, na pia kuna vyanzo vipya vya mapato 19 ambavyo havikuwapo kwenye sheria hizo.
"Rasimu iliyopitishwa ni ya mwaka 2025, lakini sheria tunazozirekebisha ni za mwaka 2018. Baada ya hatua hii, rasimu itapelekwa kwa Mkuu wa Mkoa, kisha kwa Waziri mwenye dhamana, ndipo sheria hizo zitaanza kutumika rasmi," amesema Hassan.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ngassa Mboje,baada ya kuwasilishwa kwa rasimu hiyo na kujadiliwa na Madiwani, aliwauliza kama wameridhia ambapo kwa kauli moja walitamka kuwa wameipitisha.
“Sheria hizi ndogo ni uhai wa halmashauri,”amesema Mboje.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Kalekwa Kasanga, amesema sheria hizo zitaboresha uendeshaji wa shughuli za halmashauri na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,amesema Madiwani hao wamefanya jambo la maana sana, kwa kupitisha rasimu hiyo,na kuiacha Halmashauri ikiwa katika hali nzuri.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela,amewasisitiza watendaji kwamba sheria hizo zitakapoanza kutumia wazisimamie pamoja na kukusanya mapato kwa uaminifu.
TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akizungumza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga akizungumza.
Wakili wa Serikali Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Salehe Hassan akiwasilisha rasimu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464