Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA) Taifa John Mnyika akizungumza wakati wa mkutano huo.



Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Serengeti Lucas Ngoto akizungumza wakati wa mkutano huo.
Na mwandishi wetu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA) Taifa John Mnyika katika ziara yake mkoani Shinyanga ameendeleza msimamo wa ‘No reforms, No election’ akiwataka wanashinyanga kulinda haki na utamaduni wa Chadema.
Amebainisha hayo leo Mei 16, 2025 katika mkutano wa hadhara wa wananchi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA) uliofanyika katika uwanja wa Jasko uliopo katika kata ya Ngokolo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, mkoani Shinyanga.
Mnyika amesema wako tayari kushiriki uchaguzi hata kesho endapo yatafanyika mabadiliko ya Katiba sambamba na tume huru ya uchaguzi.
“Wanaosema tunawachelewesha kupata haki zao za kugombea ubunge, chama chetu hakiko kwa ajili ya ubunge au uongozi wowote bali kipo kwa ajili ya haki, ni bora tuchelewe lakini tulinde utamaduni wa chama, na tuko tayari kushiriki uchaguzi hata kesho endapo yatafanyika mabadiliko ya katiba sambamba na tume huru ya uchaguzi” amesema Mnyika.
Mjumbe wa kamati kuu Chadema taifa Godbless Lema amesema kuwa hawajasusia uchaguzi bali wanataka haki na watawashawishi wananchi kuzuia uchaguzi kwa njia ya amani.
“Hatutaki kupendelewa tunataka haki itendeke tunawashawishi wananchi wazuie uchaguzi kwa njia ya amani wala si machafuko siku zote tunataka amani hatutaki machafuko” amesema Lema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Serengeti Lucas Ngoto amesema kuwa hawaogopi uchaguzi ila wanataka kusimamia kile kilicho haki kwa watanzania na kuwaomba wanachama na wananchi kuwaunga mkono katika mapambano ya kudai katiba mpya.

