MADIWANI WAGAWANYIKA BAADA YA MBUNGE KUJADILIWA KWENYE KIKAO CHA MADIWANI MSALALA
Na Shaban Njia, KAHAMA.
BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wamepinga vikali maadhimio ya kumuadhimia Mbunge wao Iddi Kassimu kufikishwa katika kamati ya maadili ya madiwani kuhojiwa kwa kile kinachodaiwa amekuwa akiwadharirisha kwenye mikutano ya madhara anayoifanya jimboni.
Aidha katika mgawanyiko huo kundi jingine limepinga vikali hatua hiyo kwa madai kikao kilipelekwa au kuendeshwa kihuni bila kuwa na ajenda ya kumjadili Mbunge kwenye kikao kinyume na taratibu na miongozi ya uendeshaji wa kikao cha baraza la madiwani ambapo ajenda zinaanzia kwenye vikao vya ndani ya chama (Kokasi).
Kadhalika April 30 mwaka huu katika kikao cha baraza la madiwani baadhi ya madiwani waliibua hoja juu ya Mbunge kuwadharirisha kwenye mikutano ya hadhara anayokuwa akiifanya kwenye kata zao, kutokuhudhuria vikao vya baraza mara kadhaa na kuomba afikishwe kwenye kikao cha maadaili ili akahojiwe.
Hoja hii ilimbuliwa na Diwani wa Segese, Joseph Manyala na kuungwa mkono na Diwani wa Bulyanhulu Shija Luyombya, diwani wa Mwanase Samson Masanja pamoja na diwani viti maalumu Bulyanhulu Nyagwema Mnyirwa katika kikao hicho.
Diwani wa Busangi Alexander Mihayo amepinga vikali hoja hiyo leo wakati wa kikao baina ya baadhi ya madiwani wa msalala na vyombo vya habari mjini hapa nakusema, katika kikao cha madiwani cha April 30 hawakukubaliana kwa pamoja Mbunge kwenda kuhojiwa na kamati ya maadili ya madiwani.
Amesema, baadhi yao wanaompiga mbunge ni wale ambao amekuwa akiwasimamisha mbele kwenye mikutano ya hadhara ili watoe majibu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa wananchi wao sasa wanapokosa majibu wanaona kama wanadharirishwa na kuonekana anawachonganisha jambo ambalo sio sahihi.
“Kipindi hiki tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Raisi wengi wetu tumejawa na joto la uchaguzi, tunaposimamishwa mbele ya wananchi kutoa majibu au taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye kata zetu na tukakosa majibu sahihi tunaona kama Mbunge anatudharirisha huku ni wajibu wetu kuwa na majibu ya kile tunachoulizwa”Amesema Mihayo.
Diwani mwingine wa Viti maalumu kata ya Isaka, Pily Izengo amesema, mara kadhaa amekuwa akizunguka na Mbunge kwenye kata zote wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Msalala, hakuwahi kuona wala kusikia madiwani wenzake wakidharirishwa mbele ya wananchi.
Amesema, yeye pia ni mjumbe wa mfuko wa jimbo na wanapokutana kujadili mgawanyo wake huwa wanahakikisha kila kata anapata fedha kulingana na uhitaji wake na mara kadhaa wamekuwa wakigusa ile miradi yenye changamoto kubwa iliyoibuliwa na wananchi na wamekuwa wakipokea kiasi cha Sh.milioni 79.
Nae Diwani wa Ngaya, Kisusi Ilindilo amesema, mwaka 2021 kata hiyo ilikuwa haina nishati ya umeme na Mbunge alipofanya mikutano hoja ya kwanza ilikuwa nishati hiyo na umeme upo vijijini vyote na vitongoji viwili pamoja na kituo cha afya kilichowaondolea adha wajawazito kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za kujifungua.
Diwani wa Mwalungulu aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Frola Sagasaga amesema, kikao cha April 30 mwaka huu hakikufuata utaratibu na miongozo mwa kikao, kwani ajenda zake huwa zinaundwa wakati wa kikao cha ndani ya chama (Kokasa) na kudhibitishwa wakati wa kikao cha madiwani kwa pamoja.
Amesema, wakati wa ajenda zilizoletwa kwenye kikao hicho hakukuwa na ajenda ya kumjadili Mbunge wao Iddi Kasimu kwa kile wanachodai anawadharirisha kwenye mikutano na kama ni kweli walitakiwa kuanzia kwenye vikao vya ndani ya chama ambapo pia kuna miongozi ya kuwabana wanaokwenda kinyume.
Sagasaga amesema, hata yeye aliwahi kuhojiwa mbele ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za ndani na zile za serikali kuu na kwakuwa alikuwa anamajibu haikuwa ngumu kuwaeleza wananchi hatua zinazoendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464