KATAMBI ATEMBELEA KATA ZOTE ZA JIMBO LA SHINYANGA MJINI KWA HELIKOPTA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), leo Mei 16, 2025, amefanya ziara ya kipekee kwa kutumia helikopta kutembelea kata zote 17 za Manispaa ya Shinyanga.
Ziara hiyo ilihusisha msafara wa viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa na lengo la kuzungumza na wananchi, kusikiliza changamoto zao, pamoja na kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika ziara hiyo, Katambi alieleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na afya, elimu, miundombinu, maji na uboreshaji wa mazingira ya ajira kwa vijana.
"Tunaendelea kutekeleza ahadi za Ilani ya CCM kwa vitendo. Hii ni ziara ya kuwashukuru wananchi, kusikiliza kero zao na kuhimiza ushirikiano katika ujenzi wa taifa," alisema Katambi.
Wananchi katika maeneo mbalimbali waliyotembelewa walimpongeza Mbunge huyo kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.
Ziara hiyo pia ilihusisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo, mikutano ya hadhara na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia taasisi za Serikali.
Endelea kufuatilia kwa taarifa zaidi na picha kuhusu ziara hii ya kihistoria...