Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro (kushoto)akiwa na Mkurugenzi wa Malula TV Daniesa Malula.
MALULA TV YAFANYA BONANZA LA MICHEZO VIJANA WAHAMASISHWA KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU 2025
Na Mwandishi Wetu,SHINYANGA
Malula TV imeandaa bonanza kubwa la michezo katika Kata ya Kitangili, Manispaa ya Shinyanga, likiwa na lengo la kutoa elimu kwa vijana kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, pamoja na kuhamasisha kujiepusha na matumizi ya madawa ya kulevya.
Bonanza hilo lililobeba jina la Malula Home Talents Competition lilifanyika jana kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:30 jioni, likishirikisha mamia ya vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Shinyanga.
Michezo iliyoandaliwa ni pamoja na mbio za Home Marathon, mbio za baiskeli, mashindano ya kula kilo nane za wali na maharage, pamoja na mashindano ya mpira wa miguu kwa timu sita.
Katika kila mchezo, washindi walipatiwa zawadi mbalimbali ikiwemo seti ya jezi, mipira na mahindi kwa lengo la kutambua na kuendeleza vipaji vya vijana.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro, aliipongeza Malula TV kwa mchango mkubwa katika kukuza vipaji na kuielimisha jamii ya vijana.
“Malula TV imekuwa mfano wa kuigwa, wakati vijana wengi wanashinda wakibet na kukaa vijiweni, Malula ameibuka na wazo, akalitekeleza kwa mafanikio, ni kijana mdogo lakini ana mchango mkubwa kwa jamii,” amesema Mtatiro.
Aidha, alitumia jukwaa hilo kuwasisitiza vijana kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, kwa kuhakikisha wanapiga kura na kutokuwa sehemu ya matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Malula TV Daniesa Malula,aliwashukuru vijana wa Kitangili kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki bonanza hilo, akisema wameonesha mshikamano na moyo wa kuunga mkono jitihada za wenzao.
“Vijana wa Kitangili wamevunja rekodi kwa mshikamano,ni jamii ya vijana wachache wanaothamini mafanikio ya wenzao,jambo ambalo tumelishuhudia hapa leo,” amesema Malula.
Katika hatua nyingine, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Shinyanga, Mhe. Patrobas Katambi, kwa kazi kubwa aliyofanya katika kata hiyo, akimtaja kuwa ni kiongozi kijana wa mfano nchini.
Katika kujibu risala ya Malula TV kuhusu changamoto ya ukosefu wa kamera ya kisasa yenye thamani ya Sh milioni 2, Mkuu wa Wilaya Mtatiro alisema wiki ijayo atakutana na Malula na ataoa maelekezo ya wapi fedha zitapatikana ili kamera hiyo inunuliwe na kwamba Serikali inatambua kazi yake.
Bonanza hilo pia lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na michezo, ambao kwa pamoja walitoa wito kwa vijana kuiga mfano wa Malula TV kwa kutumia vipaji na ubunifu katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.