MADIWANI SHY DC WAPONGEZA SERIKALI,WAITAKA TARURA KUBORESHA MIUNDOMBINU

Na Kareny  Masasy,Shinyanga

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga  wamepongeza  serikali kuchukua hatua kutekeleza miradi kwenye sekta mbalimbali  huku wakitaka wataalamu kuendelea kutekeleza maazimio ya kwenye vikao.

Pia wameomba  miundombinu ya barabara iendelee kuboreshwa zaidi ili wananchi  wanapokwenda kwenye shughuli zao na wafanyabiashara wasiweze kukwamishwa.

Madiwani hao wamesema hayo  leo tarehe 29/04/2025 kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani  ambapo walieleza  maazimio ya baraza lililopita walitaka miradi iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ikamilike.

Diwani wa kata ya Mwamala  Hamis Maganga amesema shule ya msingi Bugogo  ilikuwa na hali mbaya  kuta zilikuwa na nyufa lakini serikali imetoa fedha  kujenga vyumba vya madarasa viwili na ofisi moja na wanafunzi  sasa wanasoma wakiwa kwenye mazingira mazuri.

Diwani wa kata ya Iselamagazi  Isack Sengerema amesema  kuna barabara ipo katika kitongoji cha Mwabundala kuna mto ambapo linahitajika daraja ili wananchi waweze kuvuka ameiomba Wakala wa barabara mjini na Vijijini (Tarura) kuhakikisha  wanafanya matengenezo haraka.

 Diwani wa kata ya Didia  Masele Luhende amesema miundombinu ya barabara kutoka  Didia Lohumbo kwenda Solwa inachangamoto wafanyabiashara wanashindwa kufika kwenye eneo la mashine kufuata  mazao ya biashara.

Makamu Mwenyekiti wa  Halmashauri hiyo Samson Nicodemas  amewataka wataalamu waendele kufanyia kazi maagizo yanayotolewa kwenye vikao nakuyafanyia kazi. 

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  Sterwat Makali  amesema baadhi ya shule zilitembelewa na viongozi kutoka TAMISEMI ambapo shule ya msingi Bugogo tayari imeletewa fedha shilingi Milioni 52 na vyumba viwili  na ofisi ya walimu vimekamilika.

Naye Meneja wa Tarura  wilaya ya Shinyanga  Samson Pamphili amesema barabara ya kutoka  didia kwenda  Solwa yenye urefu wa kilomita 14 inafanyiwa kazi na tayari kilomita 6 imechongwa na mkandarasi   anasubiri malipo yake huku barabara ya kutoka Tinde kwenda Usule ipo kwenye mpango wa fedha za dharura.

 “ Kwa Ujumla Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  barabara  zinazopitika  vizuri ni asilimia   64.23  ambazo ziko kwenye kiwango cha wastani ni asilimia  18.75 na asilimia 17.01 ziko kwenye hali mbaya” amesema Pamphil.

 

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464