Header Ads Widget

KINANA;UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA,UCHAGUZI MKUU 2025 UTAKUWA NA USHINDANI,AWATAHADHARISHA CCM WASIBWETEKE

Kinana awaonya CCM kutobweteka uchaguzi 2025

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amesema uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani utakuwa na ushindani, hivyo wanachama wa chama hicho wasibweteke.

Kinana amesema ushindani huo unatokana na ujio wa sheria mpya za uchaguzi zilizopitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais, wanazotakiwa kuzisoma na kuzielewa vizuri kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi huo.

Akizungumza katika kikao kazi cha ndani na Wana-CCM Wilaya ya Rorya mkoani Mara, leo Jumatatu, Aprili 15, 2024 ambako anaendelea na ziara ya kichama, Kinana amesema kuna kanuni za uchaguzi za vyombo vya dola ambazo wanatakiwa kuzijua.

“Tunatakiwa tufuate maadili ya uchaguzi na tufanye kila linalowezekana na nimepata ahadi nyingi kwamba tutashinda kwenye uchaguzi unaokuja wa Serikali za mitaa mwaka huu, niwaambie utakuwa na ushindani.

“Kwa sababu zile sheria za uchaguzi zilizotungwa bungeni zinatoa nafasi ya ushindani, kwa hiyo tusibwete, badala yake tujipange vizuri. Tunatakiwa tujipange wanachama ili tupate ushindi wa kishindo mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2025,” amesema.

Kinana amesisitiza kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa ni vema wanaCCM wakashikamana na kama kuna mtu mchana yuko upande wa CCM na usiku upinzani anapaswa kuwekwa kando haraka.

“Hatuwezi kukubali watu wavae nguo za kijani mchana halafu baadaye unabadilika, hatuwezi kukubali,” amesema Kinana ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Mara.

Apiga vita ukabila

Katika hatua nyingine Kinana amewasisitiza wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kuachana na tabia za ukabila, akieleza kuwa ni mambo ya kizamani na yanawagawa.

Kauli hiyo ilikuja baada ya baadhi ya wajumbe kuibua hoja katika mkutano huo, kwamba kuna mambo yanafanyika wilayani Rorya ambayo yanaashiria kuwepo kwa changamoto ya ukabila miongoni mwao.

Kinana amesema nchi kuwa na makabila ni jambo la kawaida ila ukabila ni jambo baya, akieleza kuwa kumuhukumu mtu kwa jambo ambalo hana uwezo nalo sio sahihi.

"Sasa usimpe mtu nafasi ya uongozi kwa sababu ya kabila lake, dini au umbile usimuhukumu, hayo ni mambo ya kizamani sana, tuangalie mtu mwenye uwezo, atafanya kazi atajituma na kujitolea, mnampima kwa vigezo sio kwamba huyu ni ndugu yangu.

"Mtu mmoja kwenye kabila lako akipata cheo anakusaidia nini hasa wewe mwenyewe? Uko kijijini kule mngekuwa mnagawana mshahara sawa, kila mmoja anakuletea 300,000 kutoka kwenye mshahara wake kwa sababu ni kabila lako sawa... wekeni watu kwa uwezo," amesisitiza Kinana.

Amesema Baba wa Taifa, Julius Nyerere ametoka mkoa huo, na ni kabila dogo na ameongoza nchi kwa miaka 24, na alipendwa, aliheshimiwa, alithaminiwa na alitukuzwa sio kwa sababu ya ukabila bali ni kazi aliyokuwa anafanya, utendaji na uadilifu wake uliomfanya aheshimika Tanzania, Afrika na duniani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Patrick Chandi amesema maagizo hayo watayafanyia kazi kwa kutoa elimu ya sheria hizo mpya kulingana na utaratibu wa chama, ili wapate ushindi wa kishindo.

SOMA HAPA ZAIDI CHANZO MWANANCHI.

Post a Comment

0 Comments