Header Ads Widget

MAAFISA ELIMU NA WATENDAJI WA KATA WASISITIZWA KUSIMAMIA WATOTO KWENDA SHULE

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Ndg. Kisena Mabuba akifungua kikao kazi cha Maafisa Elimu na watendaji wa Kata kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri uliopo Kata ya Iselamagazi February 06, 2024
Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Ndg. Kisena Mabuba wakati wa kikao cha Mkurugenzi huyo na viongozi hao.
Baadhi ya Washiriki wakifuatilia kwa ukaribu wakati wa kikao cha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata.
Baadhi ya Washiriki wakifuatilia kwa ukaribu wakati wa kikao cha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata.

***


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Ndg. Kisena Mabuba amewaagiza Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata kuhakikisha kuwa watoto wote wanakwenda shule.

Maagizo hayo yametolewa leo Februari 06, 2024 wakati wa kikao kazi baina yake na Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri uliopo Kata ya Iselamagazi.


Akizungumza katika kikao hicho Mabuba amesema halizishwi na mwenendo wa kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na awali katika shule mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

“...Mkafanye kazi kwa ushirikiano kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaripoti shule walizopangiwa na wale wenye umri wa kuandikishwa elimu ya awali na msingi wanaenda shule.” Amesisitiza Ndg Mabuba


Aidha, amepiga marufuku kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kufanya kazi hususani muda wa masomo. Mkurugenzi huyo amesema viongozi hao wa kata wana wajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya matendo ya kikatili ili kupunguza na kuondoa kabisa changamoto ya ndoa za utotoni na mimba katika umri mdogo.

Maafisa Elimu na Watendaji wa kata hao wameaswa pia kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi kwa weledi na kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma akieleza kuwa uwazi na uwajibikaji ndio nguzo kuu ya utumishi.


Akizungumzia mapato na matumizi, Mkurugenzi Mabuba amewaagiza viongozi hao kuhakikisha kuwa wanafanya vikao na mikutano ya kisheria kwa kila robo ya mwaka. Mikutano hiyo itumike kama majukwaa ya viongozi na wananchi kujadili taarifa za maendeleo ya kata na vijiji pamoja na kuwasomea taarifa za mapato ,miradi ya maendeleo na matumizi ya vijiji na kata.

"Mnayo dhamana ya kusimamia ukusanyaji mapato katika kata zenu. Ni kinyume cha Sheria kukusanya fedha za Umma bila mashine ya 'POS' na kukaa na fedha za umma bila kuziweka Benki",Alisisitiza Ndg. Mabuba.

Post a Comment

0 Comments