Header Ads Widget

WANAWAKE WAJITOKEZA KUPATA CHANJO YA UVIKO- 19 SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Muuguzi wa Zahanati ya  kijiji cha Mwakata halmashauri ya Msalala  Rhobi Magambo  akitoa elimu kwa mwananchi kabla ya kumpatia huduma ya chanjo ya Uviko-19.

 Na Kareny  Masasy, Msalala

BAADHI  ya  wananchi  wa kijiji cha Mwakata   halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamehamasishana  kuchanja  chanjo ya Covid-19 katika kusherekea siku ya wanawake duniani.

Sherehe hizo  kwa halmashauri hiyo  imefanyika leo tarehe  07/03/2023  katika shule ya sekondari Mwakata ambapo Kabla ya kuanza sherehe hizo walihamasishwa  na Afisa lishe wa halmashauri hiyo Peter Ngazo  umuhimu wa chanjo hiyo ambayo ni  kinga na haina madhara yoyote.

Baada ya kumaliza kutoa Elimu ya chanjo ya Covid-19   Afisa Lishe huyo  aliuliza ambaye amechanja na  alipochanja alipata madhara gani walijitokeza waliochanja  na kueleza hakuna madhara yoyote na maisha yanaendelea.

“Tulikuwa tunadanganyana zamani kuwa  ukichanja kama mjamzito mimba inatoka au ukichanja huna mimba hutapata mtoto,kama mwanaume utakosa nguvu za kiume  Imani hiyo potofu  tuiondoe tuchanje ili tuwe salama”amesema Ngazo.

Ngazo amesema chanjo hiyo inawahusu watu wenye umri wa kuanzia miaka 18 kwani kinga zao zinaenda zikipungua tofauti na watoto kinga zao bado ziko juu hawawezi kupata madhara ukilinganisha na mtu mzima.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mwakata Mseka Mathias amesema kuna kaya 700 ambapo  wiki iliyopita kulikuwa na mkutano wa hadhara wakuhamasisha utoaji wa chanjo ya Covid-19 walijitokeza watu Zaidi ya 100 wakachanja kwa hiari yao.

Muuguzi kutoka Zahanati ya kijiji cha Mwakata  Rhobi  Magambo amesema  wanawake ndiyo wameongoza  kwa kuchanja wamehamasishana.

“Nimechanja wanawake zaidi ya 10 na mwanaume mmoja kwa haraka haraka  lakini wengi wameanza kuelewa tofauti na zamani  wamekuwa wakifuata wenyewe kwenye Zahanati huduma ya chanjo”amesema Magambo.

Mkazi wa kijiji cha Mwakata Helen Benjamin   (52)amesema  amechanja muda mrefu  na hajapata madhara mwanzo alipata hofu lakini ameona hakuna kilichomtokea nakuhamasisha wengine nao wakachanja.

Muuguzi Rhobi Magambo kutoka Zahanati ya Mwakata akitoa huduma ya chanjo ya Uviko-19.
Wahamasishaji wa chanjo  ya Uviko -19  na utoaji elimu kutoka shirika la SHDEPHA+
Wananchi wa kata ya Mwakata wakisikiliza elimu ya Uviko-19

Ofisa lishe wa halmashauri ya  Msalala Peter Ngazo akitoa elimu ya Uviko -19 kwenye  maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.Post a Comment

0 Comments