Header Ads Widget

UMOJA WA WANAWAKE UWT MKOA WA SHINYANGA WASIKITISHWA NA TAKWIMU YA ULAWITI NA UBAKAJI NDANI YA MIEZI TISA, WAKEMEA TABIA YA WANAUME WANAOFANYA TABIA HIYO


Viongozi wa Umoja wa Wanawake CCM Mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa wa dawati la jinsia baada ya kupata taarifa mbalimbali za wanawake na watoto


Suzy Luhende,Shinyanga Blog

Umoja wa Wanawake UWT CCM mkoa wa Shinyanga wamekemea vikali tabia ya wanaume wanaowalawiti na kuwabaka watoto wao wakiwemo ndugu, ambapo wamebaini jumla ya watoto 139 wamelawitiwa na kubakwa ndani ya miezi tisa, ambapo watoto 55 wamefanyiwa ukatili huo ndani ya miezi mitatu, na watoto 84 ndani ya miezi sita.

Hatua hiyo ya kukemea imekuja baada ya Umoja huo kutembelea dawati la jinsia Mkoa wa Shinyanga na kutembelea ofisi ya mwendesha mashitaka Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake na watoto Mkoani Shinyanga.

Wakizungumza na mwendesha mashtaka wa Mkoa wa Shinyanga Ajuaye Zegeli amesema ndani ya miezi sita walisikiliza kesi 84 za ubakaji na ulawiti ambazo ni za kuanzia mwezi Juni 2022 hadi Desemba 2022 na kuanzia Desemba 2022 hadi februari 2023 wamesikiliza kesi 55 ambazo zote ni za ulawiti na ubakaji.

Zegeli amesema katika Mkoa wa Shinyanga hali ya ulawiti na ubakaji imekithiri na wanaofanya vitendo hivyo ni wazazi wa kiume na ndugu wa karibu, na shida kubwa wanapokamatwa watuhumiwa, watoa ushahidi wanakwepa kutoa ushahidi kwa sababu ni ndugu wanayamaliza huko huko na watuhumiwa wanaachiwa huru wanarudi kuendeleza ubakaji na ulawiti .


"Kwa kweli hali ni mbaya sana na inasikitisha sana kwani wengi wanaofanya matukio haya na ndugu na wazazi wenyewe wanawabaka watoto wa kike na kuwalawiti, wengine wanakuwa na imani za kishirikina na wengine kwa mapezi yao, na ili vitendo hivi visiendelee elimu itolewe kuanzia makanisani misikitini, ili wananchi wasiogope kutoa ushahidi, wale wale ndio watakuwa wanarudi na kuendeleza ukatili huu,"amesema Zegeli.

Hata hivyo mwendesha mashitaka Juaye ameshauri kuwa serikali ijenge nyumba ya kuwahifadhi wahanga wanaofanyiwa ukatili na watoa ushahidi kwa ajili ya kusubiri kesi inasikilizwa kuliko kurudi nyumbani ambapo wanaporudi huko wanabadilika kwamba kama alisema aliyemfanyia ukatili ni fulani wakielewana huko ndugu kwa ndugu anakataa kuwa sio huyo ni mtu mwingine,lakini wakikaa sehemu moja na kesi ikaendeshwa kwa haraka watatoa ushahidi na mtuhumiwa atapewa adhabu yake.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Shinyanga Grace Samweli amekemea vikali tabia hiyo na kuomba jeshi la polisi liwatendee haki wanaofanyiwa ukatili huo, na kuwataka wakazi wote wa Mkoa wa Shinyanga wawe wanatoa ushahidi pindi yanapotokea matukio ya ukatili kwa wanawake na watoto, kwani bila kufanya hivyo kwa baadae hawatakuwepo wanaume wa kuzalisha na wanawake wa kuzaa.

"Nimesikitishwa sana na takwimu hizi na hizi ni wale tu waligundilika, kuna wengine sasa wamefanyiwa ukatili huu lakini hawajajitokeza, niwaombe wanajamii tujitokeze kupaza sauti ili tunusuru watoto wetu wasiendelee kubakwa na kulawitiwa hiki kitendo tusimame tukikemee kisiendelee kujitokeza na tusisite kutoa ushahidi," amesisitiza Samweli.

Katibu wa Umoja wa Wanawake UWT Mkoa wa Shinyanga Asha Kitandala amewaomba kina mama wasiwaache watoto wao wakiwa na umri mdogo wanapoachana na baba zao, kwani kuna baadhi ya wanaume wanawafanyia vitendo vibaya watoto wao, hivyo wanawake wanatakiwa kuwa makini ili kulinda watoto wasizulike.

"Hivi karibuni baba mmoja ametuhumiwa kuwalawiti watoto wake wawili wa kiume inasikitisha sana, wanaume mnaofanya hivyo mnatakiwa muwe na hofu ya Mungu tuwahurumie watoto wetu, baada ya kumsilikiza mwendesha mashtaka nimetoa machozi kabisa," amesema Kitandala.

Mjumbe wa baraza la Umoja wa Wanawake Taifa Christina Gule amelitaka jeshi la polisi lisimamie haki litoe elimu kwa wanawake ambao hawana uelewa kwani kuna wanawake wapo huko vijijini wanateseka wanafanyiwa ukatili watoto wao lakini wamekaa kimya kwa sababu hawajui kama kuna dawati la jinsia.

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Shinyanga Rehema Namanilo amesema takwimu za kufanyiwa ukatili zinatisha ni vizuri jeshi la polisi likatenda haki likasimamia ipasavyo angalau likawabana wahalifu wakapewa adhabu yao na litoe elimu kuanzia ngazi ya vitongoji ili watu hao waliokandokando ya mji wawe na uelewa wa kutoa ushahidi.

Kwa upande wao wajumbe wa kamati ya utekelezaji UWT Mkoa wa Shinyanga Hamisa Magulu na Ester Makune ambaye ni naibu Meya wa manispaa ya Shinyanga, wamesema wanawake wanatakiwa wajishughulishe waache kutegemea waume zao, ndiyo maana wanafanyiwa ukatili wanavumilia kwa sababu wanajiuliza wakiondoka na watoto watawalisha nini, lakini kama mwanamke unajishughulisha huwezi ukavumilia kupigwa na kutetea mme ambaye anamfanyia ukatili mtoto

Kwa upande wake mratibu wa Dawati la jinsia na watoto mkoa wa Shinyanga mrakibu Mwandamizi wa jeshi la polisi Monica Venance Sehere amesema kwa kweli Mkoa wa Shinyanga una matukio mengi ya ukatili wanawake wanapigwa wengine wanapoteza maisha kwa sababu wanakaa na kuvumilia kwa wanaume.

"Tuwaombe wanawake wapaze sauti wanapofanyiwa ukatili waje kwenye vyombo vya sheria kwani ni wachache tu wanaokuja katika dawati la jinsia lakini wengine wanafanyiwa ukatili wanapigwa lakini wanasema bado wanawapenda waume zao,wengine wanajiuliza wakitoka wataishije hivyo inabidi wavumilie tu vipigo,"amesema Monica.



Viongozi wa Umoja wa Wanawake UWT mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye picha ya pamoja na mwendesha mashitaka Mkoa wa Shinyanga Ajuaye Zegeli, baada ya kumaliza mahojiano

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake UWT mkoa wa Shinyanga Grace Samweli kushoto akiwa na katibu wake wa UWT mkoa Asha Kitandala katika ofisi ya mwendesha mashitaka Mkoa wa Shinyanga
Mwendesha mashitaka mkoa wa Shinyanga Ajuaye Zegeli akiwa ofisini kwake akiongea na Wanawake wa Umoja wa wanawake UWT Mkoa wa Shinyanga
Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Wanawake UWT Mkoa wa Shinyanga wakiendelea na majadiliano baada ya kutembelea ofisi ya mwendesha Mashitaka Mkoa wa Shinyanga.

Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Wanawake UWT Mkoa wa Shinyanga wakiendelea na majadiliano baada ya kutembelea ofisi ya mwendesha Mashitaka Mkoa wa Shinyanga.

Viongozi wa Umoja wa Wanawake wakimsikiliza mwendesha mashitaka akiitoa taarifa za matukio mbalimbali ya ukatili Mkoa wa Shinyanga



Post a Comment

0 Comments