Header Ads Widget

UNFPA YATEMBELEA MIRADI YA WAHANGA WA UKATILI WA KIJINSIA HALMASHAURI MSALALA WILAYANI KAHAMA

Mwakilishi mkazi wa shirikia UNFPA nchini Tanzania Mark Bryan Schreiner akizungumza na vyombo vya habari muda mfupi baada ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la kituo cha pamoja cha kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia kinachojengwa kata ya Bugharama.

Na Shaban Njia, KAHAMA.

MASHIRIKA ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania UNFPA na UNWOMEN wametembelea miradi inayotokelezwa kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoani Shinyanga inayofadhiriwa na Shirika la maendeleo la nchini Korea (KOICA).

Miradi hiyo hiyo kituo cha pamoja cha kuhudumia Wahanga wa ukatili wa kijinsia, Klabu ya wasichana ya kupinga ukatili wa kijinsia, kituo cha taarifa na maarifa, choo katika soko la Segese pamoja na kilimo cha Mboga na matunda.

Aidha miradi hiyo inatekelezwa na Mashirika ya TAHA, KIWOHEDE, TGNP, C-SEMA, Halmashauri ya Msalala, katika kata za Bugharama, Shilela pamoja na Kata ya Segese kwa lengo la kutokomeza ukatili wa kijinisia ndani ya familia na jamii huku chanzo chake kikiwa ni umasikini.

Akitoa taarifa ya ujenzi kituo cha pamoja cha kuhudumia Wahanga wa ukatili wa kijinsia kata ya Bugharama,Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali KIWOHEDE,Justa Mwaituka amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza Novemba 2021 na kinatarajia kukamilika tarehe 30 june mwaka huu na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema kituo hicho kitakapokamilika kitagharimu kiasi cha Sh.milioni 95 fedha zilizotolewa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania UNFPA na UNWOMEN kwa ufadhiri wa Shirika la maendeleo la nchini Korea (KOICA).

Amesema kituo hicho kitakuwa Ofisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Dawati la kijinsia, Afya, Ustawi wa jamii, Kamati ya Mtakuwwa ngazi ya Kata,Mhudumu wa msaada wa kisaikolojia na Ofisi ya msaada wa kisheria ili linapokea kesi kuripotiwa katika kituo hicho iweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka zaidi na kitasaidia wananchi kupata huduma karibu na makazi yao.

Naye Ofisa Ustawi wa Halmashauri ya Msalala Richard Ng'ondya, amesema richa ya kuendelea kutoa elimu ya kupinga vitendo vya kikati bado vimezidi kuongezeka kila siku na kwa mwezi yamekuwa yakiripotiwa matukio 10 hadi 15 hivyo kitakapokamilika kituo hicho na kuanza kutoa huduama kitasaidia kupunguza wimbi la matukio hayo.

Amesema vitendo vya ubakaji, ulawiti na vipigo kwa akinamama vimeshika kasi kata zote za Halmashauri ya Msalala na wengi wanashindwa kutoa taarifa kwa uwepo wa umbali wa kituo cha Polisi na Ofisa ya ustawi wa jinsia na kwamba kituo hicho kitachangia wengi kujitokeza na kupata huduma.

Aidha, Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Bugharama Dk. Silasi Kayanda amesema, wamekuwa wakipokea Wahanga mbalimbali wa matukio ya ukatili wa kijinsia na kuwapatia huduma za kitabibu na mwaka huu kuanzia januari hadi june wameshawapatia huduma Wahanga 280.

Amesema vitendo vya kikatili kwa watoto na wanawake vimeshamili katika kata hiyo na kwamba mwaka jana matukio 705 yariripotiwa na kupatiwa huduma katika kituo hicho na hizo ni takwimu za wanaojitokeza kupata huduma ukiachilia mbali taarifa zinazoripotiwa ofisi za kata na kituo cha polisi dawati wa jinsia.

Kayanda amesema,kutoka kituo cha afya mpaka kituo cha Polisi ni umbali wa kilometa tano huko ofisi za Ustawi wa jamii zikiwa umbali wa kilometa 70 hali ambayo wale wanaofanyiwa vitendo vya kikatili wanashindwa kufika vituoni kwa wakati na kukata tamaa kwa kuhofiwa kutengwa na familia zao.

Kwa upande,Mwakilishi mkazi wa shirikia UNFPA Tanzania Mark Bryan Schreiner alisema,wamekuwa wakishirikiana na serikali katika kupambana na vitendo vya kikatili ndani ya jamii nchi nzima kwa kutoa elimu ya ujasiriamali, kilimo na afya kwa sababu vitendo hivyo vinasababishwa na umasikini ndani ya familia.

Amesema,ili kuendelea kupambana na vitendo hivyo hivi karibu watajenga vituo hivyo vingine viwili katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na Shinyanga lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi ili kutokomeza vitendo hivyo ambavyo vimetajwa kuathiri wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary aliyekuwa Mgeni rasmi katika ukaguzi wa ujenzi wa kituo hicho amesema anatamani vituo hivyo vingejengwa kila kata zilizopo mkoani hapa kwani vinasaidia kupambana na matendo ya ukatili ndani ya jamii na sasa kila kituo cha afya kinachumba cha kutolea huduma hizo.

Amesema wengi wamekuwa wakifanyiwa ukatili na kushindwa kutoa taarifa kwa hatua zaidi za kisheria kwa sababu ya umbali mrefu wa vituo vya polisi,Ofisi za ustawi wa jamii na madawati ya jinsia,na kwamba kitakapokamilika kituo hicho kitasaidia kutoa huduma kwa Wahanga na kupata taarifa sahihi za watu wanaofanyiwa vitendo vya kikatili.
Mwakilishi mkazi wa shirikia UNFPA nchini Tanzania Mark Bryan Schreiner akizungumza na vyombo vya habari muda mfupi baada  ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la kituo cha pamoja cha kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia kinachojengwa kata ya Bugharama

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary akizungumza na vyombo vya habari baada ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la kituo cha pamoja cha kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia kinachojengwa kata ya Bugharama kwa Sh.milioni 95 na Mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania ambayo ni UNFPA, UNWOMEN kwa ufadhiri wa KOICA.

Moja ya jengo la kituo cha pamoja cha kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia kinachojengwa kata ya Bugharama.

Post a Comment

0 Comments