Header Ads Widget

SERIKALI YAIPA KIPAUMBELE AFYA YA UZAZI, YAONGEZA UPATIKANAJI DAWA ZA UZAZI WA MPANGO NCHINI

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Na Damian Masyenene

AFYA ya uzazi imezidi kupiga hatua na kupewa kipaumbele nchini tofauti na miaka michache iliyopita ambapo Serikali kupitia wizara ya afya imetangaza vipaumbele 13 vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 huku kipaumbele namba tatu kikiwa ni kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga pamoja na mimba za utotoni.

Akisoma hotuba ya wizara hiyo Mei 16, mwaka huu bungeni jijini Dodoma kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara ya afya kwa mwaka 2022/23, Waziri Ummy Mwalimu alisema wameendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kabla ya kujifungua, wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Alisema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 wizara kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango dozi 1,755,349 sawa na asilimia 82 ya lengo, sindano za uzazi wa mpango aina ya depo-provera dozi 2,125,625 sawa na asilimia 93 ya lengo na vipandikizi 206,000 sawa na asilimia 78 ya lengo ambapo dawa hizo zilisambazwa katika halmshauri zote nchini.

“Katika kipindi hicho wateja waliotumia njia za uzazi wa mpango walikuwa 4,189,787 ukilinganisha na wateja 4,357,151 wa mwaka 2020, vipandikizi asilimia 57.1, sindano asilimia 18.5, vidonge asilimia 10.1, kondomu asilimia 5.3, kufunga kizazi mama asilimia 0.4, Kitanzi asilimia 7.2 na njia zingine asilimia 1.4,” alisema Ummy na kuongeza;

“Njia hizo za uzazi wa mpango zilitolewa katika vituo mbalimbali vya huduma za afya nchini ambapo Serikali imeendelea kutoa elimu ya umuhimu wa akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya,”

Akizungumzia umuhimu wa afya ya uzazi kwa vijana walio katika rika balehe, Waziri Ummy alisema katika kupambana na changamoto za afya wanazokutana nazo vijana jumla ya watoa huduma za afya 650 kutoka mikoa ya Njombe, Dodoma, Morogoro, Kigoma, Tanga, Geita, Singida, Shinyanga, Iringa na Arusha wamejengewa uwezo kuhusu kutoa huduma za afya rafiki kwa vijana.

Alibainisha kuwa jumla ya vijana 397,613 sawa na asilimia 32 ya vijana balehe walipatiwa elimu na matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango huku mwongozo ukiandaliwa kuhusu namna ya kuwafikia vijana hao hususan walioko kwenye taasisi za elimu ya juu na kati.

“Vilevile, ili kupunguza changamoto za afya ambazo vijana wanakumbana nazo, mwongozo umeandaliwa wa namna ya kuanzisha program za kuwafikia vijana walioko kwenye taasisi za elimu ya juu na kati ili kutoa elimu na huduma za kujikinga na maambukuzi ya Virusi vya Ukimwi, ukatili wa kijinsia na elimu ya afya ya uzazi,” alisema.

John Maige mwanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) jijini Mwanza aliipongeza serikali kwa hatua hizo za kutambua umuhimu wa elimu ya afya ya jamii kwa vijana hasa walioko kwenye vyuo vikuu na vya kati kwani ndiyo wako kwenye hatari kubwa ya mimba zisizotarajia na magonjwa ya zinaa ikiwemo Virusi vya Ukimwi.


Post a Comment

0 Comments