Header Ads Widget

WAFAMASIA WALAANI MADUKA YA DAWA MUHIMU KUHUDUMIWA NA WATU WASIO NA TAALUMA YA DAWA WAKIWAMO WAFANYAKAZI WA NDANI


Katibu Mkuu wa Chama cha wafamasia nchini Tanzania Benson Katundu.

Katibu Mkuu wa Chama cha wafamasia nchini Tanzania Benson Katundu, akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

CHAMA cha wafamasia hapa nchini (PST), wamelaani vitendo vya baadhi ya wamiliki wa maduka ya dawa muhimu, kuweka watu wasio na taaluma kwenye maduka hayo wakiwamo wafanyakazi wa ndani na kutoa huduma kwa wananchi jambo ambalo ni hatari kiafya.

Katibu Mkuu wa Chama cha wafamasia nchini Tanzania Benson Katundu, amebainisha hayo leo Aprili 22, 2022 wakati akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga, kufuatia baadhi ya video ambazo zimesambaa mitandaoni, zikionyesha baadhi ya maduka ya dawa muhumi yakitolewa huduma na watu wasio na taaluma.

Alisema kufuatia video hizo kuonyesha madhaifu hayo, chama hicho cha wafamansia kinalaani tabia hiyo ya wamiliki wa maduka ya dawa muhimu, kuajili watu wasio na taaluma ya dawa na kuhatarisha afya za wananchi, ikiwamo kupata ulemavu na hata kusababisha kifo.

“Katika mitandao mbali mbali ya kijamii zimeonekana video kadhaa zikionyesha watoa huduma wasio na taaluma ya dawa, wakihudumia katika maduka ya dawa kinyume na miongozo, sheria na taratibu zinazosimamia maduka ya dawa muhimu, na wengine ni wafanyakazi wa ndani tu jambo ambalo ni hatari,”alisema Katundu.

“Chama cha Wafamasia Tanzania tunakemea na kulaani vikali vitendo hivyo vya maduka ya dawa muhimu kuajiri watu wasio na taaluma ya dawa, kwani ni hujuma kwa afya za watanzania ikiwa dawa isipotumiwa kwa usahihi hua inageuka kuwa sumu mwilini, na kuweza kusababisha ulemavu na hata kifo,”aliongeza.

Aidha, alisema chama hicho cha wafamasia wanaliomba baraza la famasia kuangalia upya mifumo ya ukaguzi wa maduka ya dawa muhimu nchini kote yaliyoko mijini na vijijini, ili kubaini maduka ambayo yanatoa huduma za dawa kinyume na taratibu na kuyachukulia hatua kwa ajili ya kuokoa afya za wananchi.

Aliwataka pia wafamasia kwa kila halmashauri, waongeze weledi wa kusimamia uanzishwaji wa maduka ya dawa muhimu katika maeneo yao na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, ili kuhakikisha maduka hayo yanahudumiwa na wataalamu wenye sifa za kutoa huduma za dawa.

Alisema, wameendelea kushudia utitiri wa maduka ya dawa muhimu yakiendelea kufunguliwa maeneo mengi pasipo kufuata utaratibu uliowekwa, na maduka hayo yamekuwa yakifanya vitendo visivyokubalika ikiwamo kuchomaji wa sindano za uzazi wa mpango, kuzalisha wajawazito, na kufanya vipimo vya magonjwa mbalimbali kinyume na utaratibu.

Aliendelea kufafanua kuwa maduka hayo ya dawa muhimu pia yamekuwa yakiuza dawa holela zikiwamo dawa za moto (antibiotics), ambazo haziruhusiwi kuuzwa katika maduka hayo ya dawa muhimu, ambazo zina athari ikiwamo kusababisha usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, na kuleta madhara kwenye mwili wa binadamu.

Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga, waliiomba Serikali kudhibiti tatizo hilo la maduka ya dawa muhimu kuajiri watu wasio na taaluma ya dawa, ili kunusuru afya za wananchi hasa katika maeneo ya vijijini ndiyo wapo wengi.
 
Na Marco Maduhu, SHINYANGA.

Post a Comment

0 Comments