Header Ads Widget

MGEJA; SOKO KUU LA DODOMA LIBADILISHWE JINA LISIITWE TENA JOB NDUGAI, ATAKA KUNDI LAKE LIJITATHIMINI AMTAJA POLEPOLE NA BASHIRU

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mtanzania Mzalendo Foundation Hamisi Mgeja, ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga,akizungumza na waandishi wa habari.
Muonekano wa Soko kuu la Dodoma lenye jina la aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai.
 


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MWENYEKITI wa Taasisi ya Mtanzania Mzalendo Foundation Hamisi Mgeja, ambayo inajihusisha na masuala ya haki, utawala bora na Demokrasia, ameiomba Serikali kubadilisha jina la Soko kuu la Dodoma kutoitwa tena jina la aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai.

Amebainisha hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, kuandika barua ya kujiuzulu nafasi yake.

Mgeja ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga ,amesema jina hilo linatia kichefuchefu kuendelea kuonekana kwenye Soko kuu la Dodoma, kwa madai ameinajisi nchi na kulidharirisha Taifa, kwa kumpinga Rais Samia Suluhu Hassani, juu ya mikopo ambayo inachochea maendeleo ya nchi, kutokana na ulevi wake wa madaraka.

"Kitendo alichokifanya Ndugai hata kumbukumbu zake kwenye lile Soko kuu la Dodoma Jina lake halifai kuwepo pale liondolewe kabisa, na kuweka jina jingine, sababu linatie kichefuchefu," alisema Mgeja.

Aidha, aliwataka pia watu ambao alidai kuwa ni wafuasi wa Ndugai kujithamini nafasi zao, na kuwataja baadhi majina yao, akiwamo Mbunge Hampher Polepole, na Bashiru Ally.

“Kundi hili ni baya sana linataka kufanya kama kipindi kile cha Malawi ambapo Rais alikuwa ni Mwanamke Joyce Banda, nalo linafaa kumalizwa kabisa ili nchi iache kuwa na wapika majungu na kusonga mbele kimaendeleo,”alisema Mgeja.

“Uamzi ambao ameuchukua Ndugai wa kujiuzulu ni mzuri sababu ukilikoroga lazima ulinywe, na hatukuamini maneno hayo ya kumpinga Rais juu ya mikopo kama angeyatoa yeye kulingana na nafasi yake, hivyo apishe nafasi hiyo ili watu wengine wachape kazi, na katika nchii hii historia imeandikwa kwa mara ya kwanza Spika kujiuzulu,”aliongeza.

Katika hatua nyingine Mgeja aliwataka Watanzania, kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika utendaji wake kazi wa kuwaletea maendeleo, na kupuuza maneno ya wasiopenda maendeleo.

Post a Comment

0 Comments