Header Ads Widget

UCHIMBAJI SALAMA WA MIGODI NI AJENDA YA KUDUMU - DKT. BITEKO


Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko Desemba  akizungumza na wachimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la machimbo la Nyamalimbe Makarashani lililopo Wilaya ya Geita mkoani Geita. 


Wachimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la machimbo la Nyamalimbe Makarashani lililopo Wilaya ya Geita mkoani Geita.  


 Waziri wa Madini,Dkt.Doto Biteko akipokea maelezo  ya hali ya usalama wa wachimbaji
dhahabu katika eneo la machimbo la Nyamalimbe Makarashani yaliyopo Wilaya ya Geita mkoani Geita. 

 Na mwandishi wetu.

WACHIMBAJI wa madini wametakiwa kuzingatia uchimbaji salama katika maeneo ya migodi yao ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji madini kwa tija na migodi iendelee kubaki salama.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko lDesemba 29, 2021 alipokutana na kuzungumza na wachimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la machimbo la Nyamalimbe Makarashani lililopo Wilaya ya Geita mkoani Geita.

Aidha, Dkt.Biteko amewaagiza wakaguzi wa mgodi katika machimbo hayo kuhakikisha wanaweka utaratibu wa daftari kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu kwa kusainisha majina ya wachimbaji wanaoingia na kutoka katika machimbo hayo.

“Wasimamizi wote mnaosimamia hapa, hakikisheni watu wanaoingia kwenye duara kabla hajaingia kwenye duara kuna daftari juu, limeandikwa anatoka wapi na umri wake, anapozama na kutoka anasaini tena,”amesema Dkt.Biteko.

Kuhusu umuhimu wa kulipa kodi, Dkt.Biteko amesisitiza kila gramu ya dhahabu inayopatikana ipelekwe kwenye masoko ya madini ili Serikali ikusanye kodi.

Aidha, amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Geita, Daniel Mapunda kutafuta wanunuzi wa madini ya dhahabu (Brokers) ili wasaidie kupunguza changamoto za wachimbaji kwenda umbali mrefu hadi Katoro kwa ajili ya kwenda kuuza dhahabu zao.

Kuhusu changamoto walizonazo hususani ya nishati ya umeme katika eneo hilo la machimbo, Dkt.Biteko amewahakikishia kwamba suala hilo limefanyiwa kazi kwa ushirikiano na Wizara ya Nishati ambao watafika kwa ajili ya kuwapatia umeme.

Aidha, Dkt.Biteko ameagiza mialo yote iliyopo katika maeneo ya maduara ya shughuli za uchimbaji madini yaondolewe ili zihamishiwe kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya kuweka mialo hiyo.

Akizungumzia kuhusu kulinda afya za wachimbaji, Dkt.Biteko amesisitiza wachimbaji wa Nyamalimbe kuhakikisha wanalinda afya zao kutokana  na maradhi mbalimbali.

Amesema, sehemu zenye shughuli za uchimbaji wa madini zina neema, lakini pia zina changamoto endapo mchimbaji hatazingatia taratibu za afya.

Naye, Jumanne Amani akisoma risala kwa niaba ya wachimbaji wa Nyamalinde amesema, uwepo wa mgodi katika  eneo hilo umeboresha maisha ya wakazi katika maeneo yanayozunguka mgodi huo na maeneo mengine ya watu wanaofika kujipatia kipato pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.

Ameongeza kuwa, wachimbaji wa mgodi wa mlipuko wa dhahabu wa Nyamalimbe wanaomba kupatiwa huduma ya umeme katika eneo la mgodi ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa wachimbaji na kuongeza tija.



Post a Comment

0 Comments