Header Ads Widget

MIKOA INAYOONGOZA UZALISHAJI WA CHAKULA, INAONGOZA KWA UDUMAVU"- NAIBU WAZIRI MWANAIDI

 

 

 

 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na Waandishi wa Habari wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu programu Jumuishi ya malezi, makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto, leo tarehe 10 Disemba, 2021 Jijini Dodoma.Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mwajuma Magwiza akielezea umuhimu wa vyombo ya habari katika kutekeleza programu Jumuishi ya malezi, makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wandishi wa Habari leo tarehe 10 Disemba, 2021 Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari nchini (UTPC) Abubakar Karsan akielezea kazi iliyofanywa na Waandishi wa Habari wa masuala ya watoto waliojengewa uwezo, wakati wa ufunguzi wa mafunzo Kwa Waandishi hao kuhusu programu Jumuishi ya malezi, makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto Jijini Dodoma leo tarehe 10 Disemba, 2021.

Waandishi wa Habari wanaopata mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu programu Jumuishi ya malezi, makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto wakifuatilia matukio hotuba ya ufunguzi kutoka Kwa mgeni Rasmi Mhe. Mwanaidi Ali Khamis leo tarehe 10 Disemba, 2021 Jijini Dodoma.

 Na Mwandishi wetu, Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema zaidi ya watoto milioni 2.6 wa chini ya miaka mitano wamedumaa na zaidi ya watoto 270 wa umri huo hupoteza maisha kila mwaka kutokana na lishe duni.

Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Waandishi wa habari kuhusu programu Jumuishi ya malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto leo tarehe 10 Desemba, Jijini Dodoma Mhe. Mwanaidi amesema Mikoa  inayongoza kwa upatikanaji wa chakula ndiyo ina changamoto hiyo ya lishe.

"Tanzania ni moja kati ya nchi za Afrika yenye idadi kubwa ya ya watoto wenye utapiamlo.  Idadi kuwa ya watoto hao ni katika mikoa ya Dar es salaam, Kagera, Kigoma, Mara, Dodoma, Geita, Tanga, Ruvuma, Mbeya, Morogoro na Tabora,tukumbuke baadhi ya mikoa hii ina kiwango cha juu cha upatikanaji wa chakula, programu hii inalenga kuchangia katika kumaliza changamoto ya lishe kwa watoto wetu nchini" amesema Mhe. Mwanaidi.

Amesema hivi sasa malezi na makuzi ya watoto hususani wa chini ya miaka 8 yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili, unyanyasaji, lishe duni na wazazi na walezi kufuatilia mienendo na usalama wa watoto.

Ameongeza kuwa, Serikali na Wadau mbalimbali wanaendelea na juhudi za kuhakikisha watoto wote wanakuwa na usawa katika malezi na makuzi ikiwemo kuvisimamia vituo 5274 vya malezi ya watoto, aidha, vituo 
1481 vimeanzishwa na mwaka 2021 Serikali imejenga vituo 20 Mkoani Dodoma na vituo 10 Dar Es Salaam 10 vimeandaliwa kuwawezesha watoto chini ya miaka 5 kupata malezi na uchangamshi wa awali.

Ameongeza pia vitendo vya ukatili kwa watoto vinarudisha nyuma jitihada za Serikali na Wadau kuhakikisha watoto wanakua katika utimilifu wao akitaja kwa miezi 9 kumekuwa na matukio zaidi ya 6009 hivyo Waandishi wana nafasi kubwa kushirikiana na Mamlaka nyingine kuelimisha jamii ili iweze kubadilika.  

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mwajuma Magwiza amesema Waandishi wa Habari ni kundi muhimu sana katika kupeleka taarifa kwa Jamii ikiwa wataelimishwa kwani wao pia ni sehemu ya utekelezaji.

"Tunaamini kundi hili likipata uelewa sahihi wakati huu, hata kwenye utekelezaji inakuwa kazi rahisi, Programu hii itazinduliwa tarehe 13 mwezi huu na kawaida ya Wizara huwa tunaanza kujenga uwezo kwa makundi muhimu ambayo yanatakiwa kupelekwa taarifa sahihi"Alisema

Naye mmoja wa Waandishi hao Jaliwasom Jasson ameshukuru kwa kupata elimu na kujengewa uwezo wakati wote wa utekelezaji wa masuala ya watoto na kuahidi kuendelea kufanya vema zaidi katika programu hiyo ya malezi na makuzi kwa kiwango na matokeo makubwa kwa kushirikiana na Serikali.

"Tunapokwenda kuitekeleza programu hii tunaomba tushirikishwe katika mikoa yote tukitumika vizuri nina uhakika elimu hii itawafikia Jamii na kuwekeza vizuri kwa watoto wetu"

MWISHO

Post a Comment

0 Comments