Header Ads Widget

MEYA -MANISPAA SHINYANGA:WAZAZI WASIWAKATISHE TAMAA YA KUSOMA WATOTO WA KIKE

 

 
Meya wa Mansipaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza kwenye sherehe ya kuwapongeza waalimu wa shule za Msingi Manispaa.

Naibu meya wa Mansipaa ya Shinyanga Ester Makune akitoa neno pongezi kwa waalimu wa shule za msingi Mansipaa ya Shinyanga kwa kufanya vizuri.


Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura akizungumza na waalimu wa shule za msingi Manispaa ya Shinyanga.

Suzy Luhende,Shinyanga

MEYA wa manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko amewataka wazazi kutowakatisha  tamaa ya kusoma watoto wa kike, badala yake wawatie moyo ili waweze kufaulu vizuri na kuweza kutimiza ndoto zao za maisha.

Hayo ameyasema leo kwenye sherehe ya kuwapongeza baadhi ya walimu wa shule za msingi zilizopo manispaa kwa kusimamia na kufundisha kwa bidii na kuwa ya 17 kitaifa katika mwaka 2020 sawa na asilimia 95 iliyofanyika leo katika kijiji cha Seseko manispaa ya Shinyanga.

Masumbuko amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwakatisha tamaa watoto wa kike kuwa hawawezi kuendelea na masomo, wengine kwa kupata tamaa ya kumuozesha au kumsaidia kazi za nyumbani, hivyo amewataka  waache mara moja tabia hiyo badala yake wawatayarishe vizuri ili waweze kufaulu na kuendelea na masomo ya sekondari.

"Hawa watoto wanaoenda sekondari naamini wanaenda kujifunza vitu vingi vya kielimu, hivyo tunatakiwa tuwatie moyo waende wakafanye vizuri katika masomo ya sekondari baadae waendelee mbele zaidi, sisi wazazi tusikimbilie mahali kwani mtoto akisoma baadae tutafaidika vingi kutoka kwa mtoto wa kike"amesema Masumbuko

Aidha aliwaomba walimu kuwa na upendo kwa wanafunzi wanaowafundisha, kwani wakiwa na upendo na kuwa kitu kimoja na wanafunzi wao watakuwa na ufaulu mzuri kwa sababu mwanafunzi nae atampenda mwalimu wake na kuweza kumwelewa vizuri anachofundishwa, pia wazazi ni vizuri wakashirikiana kwa karibu na walimu ili kuhakikisha mtoto anafanya vizuri.

"Nampongeza sana mkurugenzi wa manispaa hii Jomaary Satura kwa kuandaa sherehe hii ya kuwapongeza walimu kwa kufanya vizuri na kusababisha ufaulu mzuri, kwani ni Jambo la kwanza kwa manispaa yetu kufanyika jambo hili, na hii naamini itaendelea kuboreshwa zaidi, leo walimu waliofanya vizuri kwenye shule zao wamepatiwa vyeti siku zijazo watapewa motisha"amesema Masumbuko.

Kwa upande wake mkurugenzi wa manispaa hiyo Jomaary Satura amesema  lengo la serikali  ni kutokomeza kabisa hali ya kutojua kusoma na kuandika, ndiyo maana ikatolewa elimu bila malipo ili kuweza kutokomeza ujinga na kuwa na jamii yenye wasomi na waelewa, hivyo wanalengo la  kuendeleza ufaulu mzuri kila mwaka.

"Tunajifunza kwa watu waliofanikiwa mwaka 1961 wakati tunapata uhuru tulikuwa tunalingana na wajapani, waindonesia lakini wenzetu wameshatupita kwa sasa wako juu wanakuja kama wadau, hivyo na sisi tumekuja na elimu bila malipo ili watoto wetu wapate elimu bora, hivyo  kila afisa elimu, wakuu wa shule wasimamie maeneo yao ili malengo yetu ya kuwa wa kwanza kitaifa yatimie"amesema Satura

"Leo tumeamua kuwapongeza walimu wetu kwa kuendelea kufanya vizuri kwani imekuwa ya 17 kitaifa lakini pia imekuwa ya kwanza mara mbili mfukulizo,pia nampongeza mwalimu wa shule hii ya Ujamaa  Japhet Jackson kwa kujituma kufundisha kwani nilifika hapa wakati nafanya ziara zangu za kukagua miundombinu nilimkuta saa moja ya jioni yupo darasani anafundisha wanafunzi, hivyo nikaona walimu na wadau wa elimu tuje kufanya jambo letu hapa ili na walimu wengine wajifunze kitu"ameongeza.

Kwa upande wake afisa elimu manispaa ya Shinyanga Neema  Mkanga amesema  lengo lao ni kudhibiti utoro kwa walimu na wanafunzi na kuhakikisha mwalimu mkuu anatunza kumbukumbu za ufundishaji, na afisa elimu kata kuhakikisha anakagua mara kwa mara mashuleni na kuhakikisha mahudhulio mazuri, hivyo na mwaka huu 2021 wanaamini watakuwa kwenye kumi bora kitaifa.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Seseko iliyopo shule ya Ujamaa Kibushi Erick amesema elimu ni dira ya mwanafunzi hivyo wataendelea kusimamia ipasavyo ili kuhakikisha watoto wanapata ufaulu wa juu zaidi.
 
 

 
Kwaya ya Chama cha Waalimu wa Shule za Msingi Manispaa ya Shinyanga wakitoa burudani katika sherehe zilizofanyika katika kijiji cha Seseko kata ya Mwamalili Manispaa ya Shinyanga.

 
Afisa Utumishi wa Manispaa ya Shinyanga  akizungumza kwenye sherehe za kuwapongeza waalimu wa shule ya msingi wa  Manispaa ya Shinyanga.


Post a Comment

0 Comments