Header Ads Widget

CCM -KARAGWE YALALAMIKIA MITA ZA TANESCO KUWA KERO KWA WANANCHI

 

 

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, katika kikao cha kwanza cha kujadili utekelezaji wa Ilani ya CCM katika wilaya hiyo

 Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, katika kikao cha kwanza cha kujadili utekelezaji wa Ilani ya CCM katika wilaya hiyo

 Na mwandishi wetu,


Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema anakusudia kukutana na watendaji wa ngazi za juu wa Wizara ya Nishati ikiwa ni pamoja na Waziri na Naibu wake kuwaeleza adha ya uwepo wa mita za umeme zinazodaiwa kuwa feki katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera hili kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo Jumatano Desemba 15, 2021 wakati akizungumza katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, katika kikao cha kwanza cha kujadili utekelezaji wa Ilani ya CCM katika wilaya hiyo.

Waziri Bashungwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Karagwe amesema mbali na kupokea simu za mara kwa mara kutoka kwa wananchi wa jimbo lake wakieleza kushangazwa na uwepo wa mita hizo feki katika nyumba zao yeye pia ni mhathirika aliyekumbwa na kadhia hiyo.

“Mimi pia mita yangu ya umeme iligoma nikawapigia simu TANESCO walivyokuja wakasema mita yangu ni feki, wakanibadilishia, Sasa nikawa najiuliza ni wananchi wangapi wanaweza kuwapigia simu TANESCO kuelezea changamoto hiyo?” Alisema Waziri Bashungwa

Baadhi ya wajumbe katika kikao hicho wameeleza kusikitishwa na uwepo wa mita hizo feki wakisema hatua hiyo inageuka uchonganishi baina ya wapiga kura wao na serikali iliyoko madarakani.

Akijibu hoja hiyo Meneja wa TANESCO Wilaya ya Karagwe Kitila Bryson amesema hakuna mita ya umeme fake inayofungwa na TANESCO, na kuwataka wawakilishi hao wa wananchi kutoa elimu kwa wananchi kufuata taratibu zote sahihi za kufungiwa umeme kutoka mamlaka sahihi.

“Kimsingi hakuna mita mbovu, miundo mbinu ya TANESCO ni mali ya Serikali hivyo sisi kama wananchi tunapo ona jambo halijakaa sawa tuna wajibu wa kutoa taarifa katika sehemu husika, unapowasha umeme miaka mitatu bila kulipia bili elewa na hilo ni tatizo hivyo toa taarifa katika mamlaka husika” alisema Bryson

Licha ya utetezi huo kikao hicho kimeielekeza TANESCO kupitia watendaji wake kutafuta namna ya kuondoa kero ya watu au matapeli wanaofunga mita na baadae kuziondoa kwa madai kuwa ni feki hili jambo hilo lisijirudie.

Kwa mujibu wa Meneja wa TANESCO, Wilaya ya Karagwe ina vijiji 77, ambapo jumla ya vijiji 68 tayari vina umeme wakati tisa vikiwa kwenye mpango wa usambazaji wa umeme vijijini awamu ya tatu hatua ya pili.

Kikao hicho cha halimashauri kuu ya CCM Kimeipokea, kimeijadili na kuipitisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kusema kazi iendeleee.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments