Header Ads Widget

MKURUGENZI ATOA UFAFANUZI KUFUNGWA VITUO VYA KUOSHEA MAGARI (CAR WASH) SHINYANGA MJINI



Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKURUGENZI wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura, ametoa ufafanuzi juu ya sintofahamu ambayo imetokea ya kufungwa kwa baadhi ya vituo vya kuoshea Magari (CAR WASH) Mjini humo na kusababisha watu kukosa huduma za kuosha Magari yao.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii leo, amesema wamefunga vituo hivyo vya kuoshea Magari, sababu ya kutofuata taratibu za Serikali na kuweka vituo hivyo holela na kuharibu mipango mji.

Alisema walifanya Oparesheni ya kukagua vituo vyote vya kuoshea Magari katika Manispaa ya Shinyanga, na kubaini wamiliki wake hawakufuata utararibu wa Serikali kwa kupewa vibali na Afisa mipango miji, bali wameingia mikataba na wamiliki wa maeneo kitendo ambacho ni kinyume na utaratibu, na kulazimika kuvifunga.

“Manispaa ya Shinyanga tuna mpango wa kuutengeneza Mji kuwa hadhi ya Jiji, hivyo kutokana na kuwapo kwa vituo vingi vya kuoshea Magari holela, bila ya kupata vibali kutoka Halmashauri kwa Afisa Mipango Miji nikaagiza wavifunge vyote na kufuata utaratibu,”alisema Satura.

“Hatuwezi kuwa na mji ambao hauna mpangilio, Manispaa ya Shinyanga ndiyo wenye mamlaka ya upangaji mji, lakini unakuta Mfanyabiashara ameingia mkataba na Shirika la Reli (TRC), Wakala wa Barabara (TANROADS) au mtu ana kiwanja chake ana sehemu kwa mbele inawekwa CAR WARSH hilo hatulitaki bali wafike Halmashauri wapewe utaratibu,”aliongeza.

Aidha ,alisema hawajafunga vituo hivyo vya kuoshea Magari kwa maksudi kwa sababu wanafahamu vimetoa ajira nyingi kwa vijana, bali wanachotaka ni kufuatwa kwa utaratibu wa Serikali juu ya mipango miji, kwa kupata kibali na kuonyeshwa maeneo sahihi ya shughuli hizo, na siyo kuweka kila mahari na kuharibu Mji.

Nao baadhi ya wafanyabiashara ambao wanamiliki vituo hivyo vya kuoshea Magari, walilalamika kufungiwa vituo vyao ghafla bila ya kupewa maelekezo yoyote, huku wakipewa siku Tano hadi siku ya jumatatu, wawe wameshafika kwenye Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupewa utaratibu wa Serikali.
 
Na Marco Maduhu- SHINYANGA

Post a Comment

0 Comments