Header Ads Widget

JELA MIAKA MITANO KWA KUMCHOMA MOTO MTOTO ALIYEKULA BILA IDHINI

 

Na Ali Lityawi - Kahama

Mkazi wa Kata ya Nyasubi Mjini Kahama Helen Mwaka (28),amehukumiwa kwenda jela miaka mitano,baada ya kumkuta na hatia ya kumchoma moto usoni binti wa mumewe kwa kula chakula bila idhini yake.

Hukumu hiyo ilitolewa Oktoba 12,2021 na Hakimu Mkazi Mfawidhi,wa Mahakama ya wilaya ya Kahama,Fredrick Lukuna,baada ya kukubaliana na ushahidi wa upande wa Mashtaka na mshtakiwa kukiri Makosa yake hivyo kumtia hatiani.

Hakimu Lukuna alisema ametoa adhabu  hiyo ya miaka mitano jela ama faini ya Shilingi laki nne (400000/=) na fidia ya Shilingi Laki Moja (100,000/=) baada ya kukubaliana na ushahidi wa upande wa Mashtaka ambao haujaacha shaka.

Ilielezwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka Mwandamizi,Mercy Ngowi,kuwa mnamo Oktoba 4,Helen aliondoka nyumbani amepika wali kwa dagaa,aliporejea alikuta mtoto mdogo wa mumewe amepakua wali na kumaliza dagaa wote.

Ndipo Helen alipoamua kumuadhibu mtoto huyo mdogo kwa kuwa anawasha njiti na kumchoma katika paji lake la uso,na kuachwa akitaabika na majeraha hayo hadi baada ya siku mbili majirani walipobaini mtoto anateseka na kutoa taarifa katika Uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Nyasubi.

Ngowi alieleza Mahakama Uongozi wa Serikali ya Mtaa ulichukua hatua stahiki kwa kumfikisha Polisi kisha Oktoba 8 kusomewa shtaka la ukatili dhidi ya mtoto na kuiomba Mahakama imchukulie hatua Kali.

Kutokana na ushahidi huo,Mahakama ilimtia hatiani Helen na ilimpa nafasi ya kujitetea ambapo alijutia kitendo alichokifanya na kuridhia apewe adhabu Kali.

Akitoa hukumu hiyo,Hakimu Lukuna,alisema atatumikia kifungo Cha miaka mitano jela ama faini ya Shilingi Laki Nne na kutoa fidia kwa muathirika ya Shilingi Laki Moja.

Hakimu Lukuna alisema kwa kuwa Mshtakiwa ni kosa lake lake la kwanza na ameomba kupewa adhabu kali,anatoa adhabu hiyo kwa kuwa Makosa ya ukatili wa mtoto yamekuwa mengi na mara nyingi yameleta makovu ya kudumu kwa mhanga.

Post a Comment

0 Comments