Header Ads Widget

WAFUGAJI WA NG'OMBE SHINYANGA WALALAMIKIA UKOSEFU WA SOKO LA NGOZI, WAOMBA MBEGU ZA KISASA...RC TELACK AWATAKA KUBADILIKA

Mkufunzi Mkuu kutoka Vyuo vya Mifugo Tanzania (LITA), Frank Mushi (kushoto) akionyesha aina ya ngozi wakati wa kuwajengea uwezo wa kuongeza wafugaji thamani ya mnyororo wa zao la ngozi za wanyama kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) wilayani Kahama.

Na Shinyanga Press Club Blog, Kahama
Wafugaji wa ng'ombe mkoa wa Shinyanga wamelalamikia ukosefu wa masoko ya ngozi zitokanazo na wanyama wanaochinjwa, huku wakiiomba serikali kuwawezesha kupata aina bora ya mbegu za mifugo ili waweze kufanya ufugaji wenye tija na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa masoko ya bidhaa hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na wafugaji wa mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani baada ya kujengewa uwezo wa kuongeza thamani ya mnyororo wa zao la ngozi za wanyama kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) iliyofanyika wilayani Kahama.

Mmoja wa Wafugaji wa Ng'ombe wilaya ya Kahama,Charles Masaganya mbali na kukosa soko na mbegu za kisasa za ng'ombe, wanakabiliwa pia na changamoto ya uhaba wa maeneo ya malisho ya mifugo na kuiomba serikali kuwatengea maeneo hayo.

"Aina ya mifugo tuliyonayo ni mbegu ya zamani, tunaomba serikali ituletee mbegu zenye muonekano mkubwa ambao utaendana na mahitaji ya sasa ya viwanda. Ngozi hazina thamani na mara nyingi tukichuna tunaitupa, hatuna masoko ya kuuzia kuna madalali tu ambao tunauza kwa bei isiyoridhisha, hii inafanya ufugaji wetu usiwe na tija na uonekane ni ufugaji usio na faida," alisema.

Kwa upande wake, Mkufunzi Mkuu kutoka Vyuo vya Mifugo Tanzania (LITA), Frank Mushi amezitaja changamoto zinazosababisha ngozi inayozalishwa na wafugaji nchini kukosa masoko ya kimataifa kuwa ni wafugaji wengi kutojua manufaa ya ngozi na ng'ombe wengi wanaofugwa hawana tija na ng'ombe wa kienyeji wanapofika soko la dunia hawana thamani kwa sababu ngozi ni ndogo na wana nundu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha amekiri kuwa kuwa ngozi inayozalishwa wilayani humo soko lake halijulikani lilipo, hali inayoisababishia serikali kukosa mapato.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa mitano ya kimkakati ya kuimarisha mnyororo wa zao la ngozi ambayo ni Arusha, Manyara, Kagera, Geita na Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amesema kuwa serikali imedhamiria kuendeleza soko la ngozi nchini, huku akiwataka wafugaji kubadili aina ya ufugaji kwani kwa sasa ng'ombe waliopo mkoani humo wana alama nyingi zinazoharibu ngozi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza katika hafla hiyo
Mfugaji wa Ng'ombe wilaya ya Kahama,Charles Masaganya akieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo na kusababisha bidhaa za ngozi kukosa thamani na masoko
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akizungumza kwenye hafla hiyo

Post a Comment

0 Comments