Header Ads Widget

RUWASA YAZINDUA MRADI WA MAJI IHAPA-SHINYANGA, DC MBONEKO AWAHAKIKISHIA WANANCHI UPATIKANAJI MAJI

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akifurahia na kunawa maji baada ya kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha Ihapa kata ya Old Shinyanga wilayani humo, uliotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Shinyanga na utanufaisha zaidi ya wananchi 3,000.

Na Damian Masyenene, SHINYANGA
WANANCHI 3,535 wa vitongoji vitano vya kijiji cha Ihapa Kata ya Old Shinyanga wilayani Shinyanga, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria uliojengwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kijijini hapo na kuondokana na kero ya muda mrefu ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na kukwamisha shughuli za uzalishaji mali.

Wananchi hao watanufaika na mradi huo ambao umezinduliwa rasmi jana Aprili 30, 2021 kijijini hapo na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, huku ikielezwa kuwa awali wananchi hao walikuwa wanalazimika kutembea umbali wa Km 4 kutafuta huduma ya maji na kusababisha kuzorotesha shughuli za uzalishaji mali na kuzusha migogoro kwenye familia.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, amewahakikishia wananchi hao kuwa miradi yote ya maji inayotekelezwa katika wilaya hiyo itakamilika na kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

Mboneko ameipongeza RUWASA kwa kuhakikisha wananchi wa kijiji hicho wanapata maji na kumtua mama ndoo kichwani, huku akiwashukuru wananchi kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa kuruhusu miundombinu ya mabomba kupitishwa kwenye mashamba yao na hatimaye mradi kukamilika.

Katika kuhakikisha mradi unakuwa na manufaa kwa wananchi, DC Mboneko amewataka wasimamizi wa mradi kuhakikisha wanadhibiti matumizi ya vishoka katika kuunganisha wananchi na huduma ya maji, huku akiwaagiza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA) kuona uwezekano wa kupiga kambi ama kufungua ofisi ya muda ili kutoa huduma ya kuwaunganisha wananchi na huduma hiyo kwa haraka na unafuu.

"Wenyeviti wa vitongoji msaidie kudhibiti vishoka, watakaopewa majukumu ya kusimamia magati wasiwe wasumbufu na kuleta foleni na malalamiko, na fedha zitakazokusanywa kutokana na maji haya kupitia kamati za maji zitunzwe vizuri na kamati hizo zisimamie vizuri," ameagiza.

Akieleza namna mradi huo ulivyotekelezwa, Meneja wa RUWASA wilaya ya Shinyanga, Emaeli Nkopi amesema kuwa mradi huo wenye thamani ya Sh. Milioni 177.9 ulianza kutekelezwa Novemba, mwaka jana umekamilika kwa asilimia 100 na sasa kazi iliyobaki ni kuukabidhi kwa SHUWASA kwa ajili ya uendeshaji, ambapo utanufaisha wananchi 3,535 wa vitongoji vitano vya kijiji cha Ihapa.

"Manufaa ya mradi huu ni kuwaondolea kero ya upatikanaji maji safi na pia wananchi kutumia muda wao kwenye shughuli za uzalishaji maji....wakati wa utekelezaji tulikutana na changamoto nyingi ikiwemo miamba wakati wa kuchimba mitaro ya kulaza mambomba," amesema.

Diwani wa Kata ya Old Shinyanga, Enock Lyeta, ameiomba SHUWASA kuona uwezekano wa kufanya punguzo la bei wakati wa kuwaunganishia huduma wananchi ili waweze kupata huduma wengi na kwa bei rafiki.

Mmoja wa akina mama katika kijiji hicho, Zena Ibrahim amesema kutoka na kukosa maji ya uhakika, walishindwa kutunza familia zao na kuleta mivurugano hali ambayo ilipelekea majukumu mengine ya kifamilia na uzalishaji mali kupwaya, hivyo huduma hiyo mbali na kuleta maelewano ndani ya familia itawapunguzia wanawake manyanyaso na mahangaiko.

Naye, Mwenyekiti wa Sungusungu tawi la Ihapa, Mzee Jiganza Chidula amemhakikishia Mkuu wa wilaya kuwa wataimarisha ulinzi kwa ajili ya kuitunza miundombinu ya maji na mradi huo kwa ujumla.

Mbali na kuzindua mradi huo, DC Mboneko pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya usalama ya wilaya na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo walikagua pia miundombinu na maji na mradi wa maji wa Kijiji cha Mwamashele kata ya Kizumbi unaotekelezwa na RUWASA.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati) akitoa maelekezo wakati akikagua miundombinu ya maji inayojengwa na RUWASA katika kijiji cha Mwamashele kata ya Kizumbi wilayani humo.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Shinyanga, Emaeli Nkopi (aliyenyoosha mkono) akimuonyesha baadhi ya miundombinu ya maji inayojengwa katika kijiji cha Mwamashele kata ya Kizumbi
Meneja wa RUWASA wilaya ya Shinyanga, Emaeli Nkopi akiendelea kuonyesha miundombinu ya maji wanayoijenga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akiburudika na wananchi wa kijiji cha Ihapa wakati akiwasili kuzindua mradi wa maji kijijini hapo
DC Mboneko akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ihapa wakati wa hafla ya kuzindua mradi wa maji unaotekelezwa na RUWASA wilaya ya Shinyanga
Meneja wa RUWASA wilaya ya Shinyanga, Emaeli Nkopi akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya Mkuu wa wilaya (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi jana katika kijiji cha Ihapa
Diwani wa Kata ya Old Shinyanga, Enock Lyeta akizungumza kwenye hafla ya kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha Ihapa kilichopo kwenye kata hiyo
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa SHUWASA, Mwandumbya Ruben akizungumza kwenye hafla hiyo
Afisa Habari wa Mamlaka ya Maji Kahama-Shinyanga (KASHUWASA), Dk. Peter Mwidima akitoa salamu za mamlaka hiyo katika hafla ya uzinduzi wa maji kijiji cha Ihapa
Mwenyekiti wa Sungusungu tawi la Ihapa, Jiganza Chidula akizungumza kwenye hafla hiyo
Mkazi wa kijiji cha Ihapa, Zena Ibrahim akieleza namna mradi huo utakavyowaondolea akina mama na mabinti kero na manyanyaso
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati) akizungumza kwenye uzinduzi huo
DC Mboneko akikata utepe kuashiria kufungua mradi huo
DC Mboneko akizindua rasmi mradi wa maji Kijiji cha Ihapa unaotekelezwa na RUWASA wilaya ya Shinyanga
DC Mboneko akifungulia maji wakati akizindua mradi huo
DC Mboneko akifungulia maji na kuwaonyesha wananchi maji watakayoanza kuyatumia kutoka kwenye mradi huo
DC Mboneko akimtwisha ndoo yenye maji mkazi wa kijiji hicho baada ya kuuzindua rasmi mradi wa maji kijiji cha Ihapa
DC Mboneko akifuarhia wakati akimtwisha ndoo ya maji mmoja wa akina mama wa kijiji hicho, ikiwa ni ishara ya kuwatua na manyanyaso ya kutafuta maji umbali mrefu
Mkazi wa kijiji cha Ihapa akifurahia wakati akitwishwa ndoo ya maji na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko
DC Mboneko akimtwisha ndoo ya maji kijana wa kijiji cha Ihapa na kuwasisitiza wanaume kuwasaidia wake zao kuchota maji
Wananchi wakiyafurahia maji baada ya kuzinduliwa kwa mradi
DC Mboneko akipiga picha ya pamoja na viongozi wa chama, wananchi na meneja wa Ruwasa baada ya uzinduzi wa mradi huo
Picha ya pamoja na wawakilishi wa RUWASA, SHUWASA na Kashuwasa
Akinamama na watoto wa kijiji cha Ihapa wakifurahia katika picha na DC Mboneko
DC Mboneko katika picha ya pamoja na baadhi ya vijana wa kijiji cha Ihapa
Wananchi wa kijiji hicho wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji
DC Mboneko akiwasisitiza wananchi kulinda miundombinu ya maji mara baada ya kuzindua mradi huo





Post a Comment

0 Comments