Header Ads Widget

MADIWANI SHINYANGA DC KUMSHTAKI MRAJISI VYAMA VYA USHIRIKA AKIDAIWA KUWAIBIA WAKULIMA....WAHOJI LESENI YA MWEKEZAJI MWAKITOLYO

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ngasa Mboje akisisitiza mambo mbalimbali wakati akizungumza na madiwani na watendaji wa serikali katika kikao cha robo ya tatu ya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo leo Iselamagazi, Shinyanga

Na Damian Masyenene, Shinyanga
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamecharuka baada ya kupata majibu yasiyoridhisha kutoka ofisi ya mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Shinyanga kufuatia kuwepo kwa vitendo vya wizi wa mauzo ya wakulima wa choroko, hivyo baraza hilo likamwagiza Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ngassa Mboje kumshtaki mrajisi wa vyama vya ushirika kwa niaba ya wakulima hao.

Hayo yamejiri leo Mei 7, 2021 katika kikao cha robo ya tatu ya baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichohudhuriwa na wataalam mbalimbali kutoka taasisi za serikali, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba.

Hoja hiyo iliibuliwa na Diwani wa Kata ya Pandagichiza, Charles Kabogo ambaye alitaka kufahamu ni lini malipo ya awamu ya pili yatafanyika kwa wakulima wa choroko wilayani humo baada ya kuahidiwa kutokana na zoezi la vyama vya ushirika na wafanyabiashara kukusanya mauzo yao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Akitoa majibu juu ya suala hilo, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Boniphace alishindwa kueleza bayana juu ya malipo hayo na kukanusha uwepo wa wafanyabiashara na vyama vya ushirika kukusanya mazao ya wakulima, huku akisistiza kuwa maelekezo ya serikali juu ya stakabadhi ghalani hayaruhusu wafanyabiashara ama vyama vya ushirika kukusanya mazao ya wakulima na kuyauza.

Hilda aliongeza kwa kuonyesha kushangazwa ni wapi wafanyabiashara na vyama hivyo vya ushirika vimepata fedha za kukusanya mazao ya wakulima na kuyauza badala ya kupeleka ghala kuu kwa ajili ya mnada.

Majibu hayo yalimnyanyua Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ngassa Mboje na kueleza kuwa mfumo huo umefanya wakulima waibiwe na mazingira hayo ya wizi yametengenezwa na ofisi ya mrajisi wa vyama vya ushirika, hivyo kwa niaba ya madiwani watamshtaki mrajisi huyo ili awalipe wakulima hao.

Mboje amesema kuwa katika utaratibu huo halmashauri inapata asilimia 30 ya mauzo, Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU) asilimia 15, huku vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) vikipata asilimia 35 ambayo mwenyekiti huyo amehoji kuwa wanaipata kwa kazi gani wanayoifanya.

Pia ameeleza kuwa kabla ya utaratibu huo uliowekwa na mrajisi, bei ya choroko ilikuwa Sh. 1,600 lakini kwa sasa imeshuka hadi Sh. 800 kutokana na urasimu huo, ambapo ameiomba ofisi ya Katibu tawala wa mkoa (RAS) kulichukua suala hilo na kulifanyia kazi.

“Itabidi tuwapeleke mahakamani kwa sababu mmetengeneza mnyororo wa wizi na tujue ni utaratibu gani mlioutengeneza kwa kuwaibia wakulima, kwanini mnakamata wakulima barabarani mpaka sasa choroko zimejaa majumbani.

“Tunao ishahidi wa miamala ya fedha ilivyokuwa ikifanyika na mnawachezea wakulima wetu, walijishusha sana lakini wameumizwa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba amesema kuwa katika zao la choroko maelekezo yalikuwa stakabadhi ghalani lakini pia wafanyabiashara waliruhusiwa, kwahiyo walitekeleza kwa mujibu wa miongozo bahati mbaya utekelezaji huo uliingia dosari, hivyo hawezi kutengua maamuzi ya baraza hilo kwani uamuzi huo ni kwa maslahi mapana ya wakulima.

“Mfumo ulikuwa ni nzuri lakini umekumbana na changamoto kubwa, imebainika kuwa Amcos wamekuwa madalali wa wafanyabiashara, wakajikuta na wao wananunua katika mfumo usio rasmi na kufanya wafanyabiashara kujikuta hawapati haki yao.

“Hii tumeichukua kama changamoto kwahiyo awamu ijayo tutazitumia hizi changamoto kama fursa ili kuona namna gani mkulima ananufaika,” amesisitiza.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Boniphace

Katika hatua nyingine, madiwani hao wamehoji uhalali wa leseni ya mwekezaji wa madini ya Dhahabu katika eneo la Mwakitolyo na ni lini uzalishaji utaanza rasmi ili halmashauri hiyo iweze kunufaika, kwani amekuwa na kisingizio kwamba anafanya utafiti jambo ambalo limedumu kwa muda mrefu.

Madiwani hao waliiomba ofisi ya madini kufanya nao kazi kwa ukaribu kwani mara kadhaa wamekuwa wakijibiwa kuwa mambo hayo (ya madini) hayawahusu.

Akijibu hoja hizo, Afisa Madini mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Joseph Kumbulu amesema kuwa leseni ya utafiti waliyokuwa wamepewa kampuni ya Zhen imekwisha na sasa wamepewa leseni ya uchorongaji na uandaaji wa njia kwa ajili ya kuchukua dhahabu, huku akibainisha kuwa tayari kampuni hiyo imemuandikia barua mkuu wa mkoa huo na kueleza kuwa ifikapo Agosti mwaka huu uzalishaji utaanza rasmi, kwani kwa sasa wanamalizia ujenzi wa tanki la maji taka.

“Kwa hili suala naomba tumvumilie, ukifika muda (Agosti) alioahidi ndiyo tutamhoji. Sisi kama wataalam tumejiridhisha kuwa mawe yanayotoka pale hayana dhahabu na kila mara wataalam kutoka tume ya madini hufika kujiridhisha,” ameeleza.

Akitoa salamu za mkoa kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Alphonce Kasenyi ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa bajeti ya fedha zilizotolewa mwaka 2020/2021 zitumike kabla ya Juni 31, mwaka hu una miradi itekelezwe kwa wakati kama ilivyopitishwa na madeni yote ya fedha za wazabuni yalipwe ili fedha hizo zisirejeshwe hazina.

Pia amesema kuwa halmashauri za mkoa huo hazijajibu hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo amezitaka kujitahidi kujibu hoja hizo na kuzimaliza.

Katika hatua nyingine, madiwani hao wameiomba Tarura kufanya mchakato wa kuihamisha barabara ya Didia-Solwa yenye urefu wa Km 55.3 ambayo matengenezo yake yatagharimu Sh Bil 1.2 ili iweze kupitika muda wote, ipelekwe kwa wakala wa barabara nchini (Tanroads) ili kuipunguzia mzigo Tarura ambao wameelemewa kwa kuwa na mtandao mkubwa wa barabara huku wakiwa na bajeti finyu.

Baraza hilo pia limeiomba ofisi ya Mkuu wa wilaya kupitia jeshi la polisi kuacha ukamataji wa pikipiki na wananchi siku za mnada hususan Tinde na maeneo mengine kwani wamekuwa wakivuruga minada kwa kuzorotesha na kuharibu ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.

Madiwani wameshauri ukamataji huo ufanyike siku za kawaida na watendaji wa ofisi ya Bima waombe vibali kwa mkurugenzi wa halmashauri watoe kwanza elimu maeneo ya vijijini kwa wamiliki wa vyombo vya moto juu ya umuhimu wa bima na kutoa muda maalum wa ukataji wa bima hizo.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Ngasa Mboje (Katikati) akizungumza katika kikao hicho. Kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri, Isack Sengerema
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba akifafanua hoja mbalimbali katika kikao hicho
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Ngasa Mboje (Katikati) akizungumza katika kikao hicho. Kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri, Isack Sengerema
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela (katikati) pamoja na viongozi mbalimbali wakifuatilia kikaohicho
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela akiwasilisha salamu za chama katika kikao hicho
Watendaji na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za serikali wakiwa ni sehemu ya kikao hicho kwa ajili ya kutolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali kutoka kwa madiwani
Diwani wa Kata ya Lyamidati, Veronica Ndutwa akiuliza swali kwenye kikao hicho
Diwani Edward Maganga akihoji mambo mbalimbali kwenye kikao hicho
Diwani wa Kata ya Nyida, Selemani Segereti akiulizwa swali wakati wa uwasilishaji wa taarifa mbalimbali kwenye kikao hicho
Diwani wa Kata ya Salawe, Joseph Buyugu akichangia kwenye taarifa iliyowasilishwa na Tarura
Diwani wa Kata ya Mwantini, Mpemba Jilungu akihoji utozwaji faini katika msitu wa Mwantini usiozingatia sheria ikiwemo kutotoa risiti
Diwani wa Kata ya Didia, Richard Masele akichangia hoja kwenye kikao hicho
Diwani wa kata ya Ilola, Amosi Mshandete akihoji kwanini zahanati ya Mendo haina mtumishi hata mmoja baada ya aliyekuwepo kustaafu
Madiwani wakipitia ripoti mbalimbali zilizowasilishwa kwenye kikao hicho
Kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea
Madiwani wakiendelea na kikao
Kikao kikiendelea
Mwakilishi ofisi ya RAS, Alphonce Kasenyi akiwasilisha salamu za mkoa
Afisa Madini Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Joseph Kumbulu akifafanua hoja mbalimbali zilizowasilishwa na madiwani
Meneja wa RUWASA wilaya ya Shinyanga, Emaeli Nkopi akiwasilisha taarifa ya wakala huo na kupongezwa na madiwani kwa kazi kubwa ya utekelezaji na kufikisha huduma ya maji safi maeneo ya vijijini
Mwakilishi wa Meneja wa TARURA wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Dominic Kajoro akiwasilisha taarifa ya wakala huo
Mwakilishi idara ya uhamiaji akiwasilisha taarifa ya idara hiyo
Mwakilishi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Kamira Beda akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali kuhusu ofisi hiyo



Post a Comment

0 Comments