Header Ads Widget

BABA ADAIWA KUMUOZESHA BINTI YAKE ANAYESOMA KIDATO CHA PILI KWA MAHARI YA NG'OMBE 6

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba

Na Damian Masyenene, Shinyanga
VITA dhidi ya Ukatili kwa wanawake na watoto inazidi kushamiri mkoani Shinyanga ili kuhakikisha kuwa ndoto za wasichana hazikatizwi kwa sababu ya mimba ama ndoa za utotoni.

Hili linaendelea kujidhihirisha baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kufanikiwa kuzuia jaribio la kumuozesha mwanafunzi wa kidato cha pili kwa mahari ya ng'ombe sita na fedha Sh. 200, 000 katika kijiji na Kata ya Usanda tarafa ya Samuye, halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani humo.

Ambapo, Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kosa la kumuozesha mwanafunzi kidato cha pili (jina linahifadhiwa), ambao ni Masele Kuyela Kusamba (52)  ambaye ni baba wa binti na Hamis Langa (30) wote wakazi wa kijiji cha Manyada.

Akitoa taarifa hiyo leo kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba alisema mnamo Aprili 28, mwaka huu saa 9:30 alasiri huko katika Kijiji na Kata ya Usanda, Tarafa ya Samuye, halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Afisa Maendeleo ya Jamii wa kata hiyo alipata taarifa ya kuozeshwa kwa mwanafunzi huyo nyumbani kwao kijiji cha Usanda ambako kikao cha kupanga mahari kilikuwa kinaendelea kufanyika ndipo alitoa taarifa kituo cha polisi mkoa wa Shinyanga na askari walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Kamanda Debora amebainisha kuwa katika kikao hicho cha kupanga mahari, watuhumiwa hao walikubaliana mahari ya ng’ombe sita na fedha taslimu kiasi cha Sh. 200,000 ambayo ilitakiwa kutolewa mwezi Mei mwaka huu.

Ameongeza kwa kueleza kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Katika kuhakikisha jitihada za kukomesha vitendo hivyo zinazaa matunda na kuwanusuru watoto wa kike na ndoa za utotoni mkoani hapa, ACP Magiligimba ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kutoa taarifa zinazohusiana na vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia kwa jeshi la polisi ili vikomeshwe.




Post a Comment

0 Comments