Header Ads Widget

RAIS SAMIA AAGIZA VYOMBO VYA HABARI VILIVYOFUNGWA VIFUNGULIWE, MAAFISA ARDHI WADHIBITIWE....ATAKA TATHMINI YA MITAALA IFANYIKE


Rais Samia Suluhu Hassan

Na Damian Masyenene
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa maagizo kwa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungwa bila kufuata sheria vifunguliwe mara moja na kusimamiwa ili vifuate sheria, miongozo na kanuni.

Vile Vile, Rais Samia ameitaka wizara hiyo kutotumia mabavu (nguvu) katika kuchukua hatua za kufunga vyombo vya habari, huku akiitaka kuvisimamia na kuhakikisha vinafuata sheria, miongozo na kanuni zilizowekwa.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Aprili 6, 2021 Ikulu Dar es Salaam wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu, Manaibu katibu wakuu wa wizara mbalimbali na wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali walioteuliwa Aprili 4, mwaka huu.

"Naskia kuna 'vitivii' (Televisheni) vya mkononi mmevifungia, vifungulieni.Vyombo vya habari mlivyovifungia mvifungulie na wafuate sheria, tusifungie tu kibabe, wafungulieni lakini tuhakikishe wanafuata miongozo na kanuni za serikali," amesisitiza. 

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameigusia wizara ya Ardhi na maendeleo ya makazi na namna ambavyo kumekuwa na uporaji mkubwa wa Ardhi kupitia maafisa Ardhi.

Rais Samia ameitaka wizara hiyo kusimamia umiliki halali wa ardhi kwa taasisi na watu binafsi na kuhakikisha mambo hayo yanaondoka, huku akiagiza kudhibitiwa kwa maafisa ardhi mikoani na wilayani kwani wanafanya mambo kwa namna watakavyo.

Kwa upande wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Rais Samia ameitaka kufanya tathmini ya elimu itakayomsaidia Mtanzania kujikwamua baada ya kuhitimu masomo yake, huku akimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kahama mkoani Shinyanga, Jumanne Kishimba kwa namna ambavyo amekuwa akitoa hoja zenye mashiko juu ya elimu bungeni.

"Wizara iangalie upya namna ya kuwasaidia watanzania na kuangalia upya mitaala ambayo itaipeleka nchi mbele. Pia historia ya Tanzania na utumiaji wa lugha ya kiswahili kwenye elimu yetu liangaliwe vizuri," amesisitiza.



Post a Comment

0 Comments