Header Ads Widget

RAIS SAMIA ATOA MSIMAMO KUHUSU COVID-19, ASHAURI TAIFA LIWE NA MSIMAMO

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Na Damian Masyenene

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa msimamo juu ya ugonjwa wa Corona (COVID-19) na kueleza kuwa ataunda kamati ya wataalam waliangalie kwa upana wake kitaalam kisha waishauri Serikali, huku akisisitiza kuwa kama taifa halipaswi kuwa kimya ni vyema wakalikataa ama kulikubali bila kufanya tafiti za kitaalam.

Rais Samia ametoa msimamo huo leo Ikulu Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha makatibu wakuu, manaibu katibu wakuu na wakuu wa taasisi za serikali walioteuliwa hivi karibuni.

“Tutaunda Kamati ya Wataalamu kuhusu Covid 19 watuambie kitaalamu hayo yanayopendekezwa na Ulimwengu kuja kwetu yapoje, hatuwezi kujitenga tu kama Kisiwa na hatuwezi kupokea yanayoletwa bila kuweka cha kwetu, bila kufanya utafiti wa kwetu,” ameeleza.

Katika hatua nyingine akitoa maagizo kwa wizara ya afya, Rais Samia ameitaka wizara hiyo kupitia wataalam wake kulimaliza suala la bima ya afya kwa wote na kulipeleka serikalini na limalizwe maramoja. 

"Wataalam wamalize hili watuletee serikalini tulimalize kwa pamoja. Watanzania wanakata bima za afya wakifika hospitalini dawa hakuna, nendeni mkalitazame hili," amesema.

Vilevile, Rais Samia amegusia suala la upungufu wa dawa MSD na kuitaka TAMISEMI kulishughulikia mara moja kwani kumekuwa na upoteaji wa dawa kabla hazijafika hospitalini.

"Huenda Tamisemi mna madeni, au dawa zinapotelea katikati.... waganga wafawidhi, wa wilaya na mikoa kuna dawa zinapotea hapo katikati chukueni hatua msioneane aibu," amesisitiza.



Post a Comment

0 Comments