Header Ads Widget

BALOZI KATTANGA AELEZA ALIVYOPATA TAARIFA ZA UTEUZI AKIJIANDAA KWENDA JAPAN...NDUGAI AWATAHADHARISHA MAWAZIRI

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga

Na Damian Masyenene
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga ameapishwa leo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, huku akieleza namna alivyopata taarifa za uteuzi wake wakati tayari amekwishakata tiketi ya kurudi nchini Japan kuendelea na majukumu yake ya ubalozi.

Uteuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Kattanga ulitangazwa jana kwa ghafla na Rais, Samia Suluhu Haasan saa 9 Alasiri Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati wa kuapishwa kwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Akieleza namna alivypata taarifa za uteuzi wake, Balozi Kattanga, amesema kuwa alifuatwa na watu kisha kupelekwa uwanja wa Ndege kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Dodoma bila kuambiwa kilichopo, huku tayari akiwa ameshakata tiketi ya kurejea Japan ambako alitakiwa kuondoka leo.

"Leo ilikuwa nirudi Japan na tiketi ile bado ninayo, ikabidi nihairishe kwa sababu jana majira ya saa 6 (mchana) hivi nikachukuliwa hadi Airpot na kuchukua tiketi nikaambiwa mambo mengine utajua huko Dodoma, bahati nzuri nikiwa Airpot nikatazama television nikajua," ameeleza. 

Balozi Kattanga amebainisha kuwa katika kuhakikisha kuwa Serikali inafanya kazi pamoja kwa mpangilio unaoeleweka, atafanya kazi kwa bidii kuondoa changamoto iliyopo Serikalini ya kukosa muunganiko katika wizara na taasisi zao pamoja na kuepusha migogoro na mivutano baina ya watumishi wa Serikali.

"Jambo muhimu, kazi ya katibu mkuu kiongozi ni kuratibu na kuunganisha wizara na taasisi zake zifanye kazi kwa ufanisi katika utekelezaji wa kazi. Nafikiri kazi yangu Mhe. Rais ni kazi yenye changamoto, lakini serikali ambayo inafanya kazi kwa pamoja na kushirikiana ni serikali inayofanya kazi kwa ufanisi, nitafanya kwa maelekezo na maagizo yako na kwa mujibu wa kiapo changu," amesema.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewaomba watumishi wa umma hususan mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao kuchapa kazi kwani Rais hatabiliki.

"Nawaibia siri ndugu zangu, mama hatabiriki, chapeni kazi," amesema. 

Naye, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewapongeza wateule wote na mawaziri ambao wameaminiwa, ambapo ameahidi kuendelea kuwasimamia vyema ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.

"Nashukuru sana kwa kuendelea kuniamini, nami nitaendelea kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na bidii kwa uaminifu ili serikali iweze kufikia malengo, na nipo tayari kufuata maelekezo yako," amesema.
Post a Comment

0 Comments