Header Ads Widget

DC MBONEKO ARIDHISHWA NA KASI UJENZI WA KITUO CHA POLISI MACHIMBONI MWAKITOLYO

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, Mkurugenzi wa  Halmashauri ya Wilaya hiyo, Hoja Mahiba pamoja na Mkuu wa Polisi wilaya ya Shinyanga, John Kafumu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa umoja wa wachenjuaji wa Dhahabu Mwakitolyo mara baada ya kumaliza kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Polisi Mwakitolyo. 

Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo cha Polisi kilichopo kwenye machimbo ya Dhahabu Mwakitolyo wilayani Shinyanga, ambacho kitasaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo.

Mboneko amebainisha hayo leo alipofanya ziara kwenye machimbo hayo kukagua ujenzi wa kituo hicho ambacho kimejengwa kwa nguvu za umoja wa wachenjuaji wa madini ya dhahabu wa Mwakitolyo (UWADHAMWA) kwa kuchangishana pesa, kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama kwenye eneo hilo.

Amesema anapongeza sana umoja huo wa wachenjuaji wa madini ya dhahabu kwa kuitikia agizo lake na kuamua kuanza ujenzi wa kituo cha Polisi kwenye machimbo hayo, ambacho ni muhimu sana kutokana na shughuli zao za uchimbaji wa madini, kwa kuwahakikishia amani inatawala kwenye maeneo hayo na hakuna uvunjifu wa amani tena.

“Kituo hiki cha Polisi kwenye maeneo hayo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu, kitakuwa msaada mkubwa pamoja na wananchi kuwahakikishia ulinzi na usalama, ambapo zamani likitokea tukio la uharifu kupata huduma hadi salawe au Shinyanga mjini zaidi ya kilometa 100, lakini kwa sasa huduma mtaipata hapa hapa,” anasema Mboneko.

“Kutokana na kunifurahisha hatua hii mliyofikia ya ujenzi wa kituo hiki cha Polisi, na mimi nilitafuta wadau ili kuwaunga mkono kukamilisha ujenzi huu, ambapo nilipata wadau kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na wamenipatia Sh. Milioni 10, na nimeshaikabidhi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga,” ameongeza.

Aidha amesema kukamilika pia kwa ujenzi huo wa kituo cha Polisi, kutatoa fursa kwa wafanyabishara na wawekezaji kuwekeza kwenye mgodi huo wa Mwakitolyo, pamoja na Taasisi za kifedha kusogeza huduma kwenye maeneo hayo, wakiwamo TRA kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.

Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Shinyanga, John Kafumu, amesema kituo hicho cha Polisi kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uharifu kwenye maeneo hayo yakiwamo ukatwaji wa mapanga, sababu Askari Polisi watakuwa doria masaa 24 ili kuhakikisha amani inatawala.

Aidha Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Madini ya Dhahabu Mwakitolyo, Aphonce Paulo, amesema walikuwa na hamu sana ya kupatiwa kituo cha Polisi kwenye maeneo hayo kutokana na usalama kuwa hafifu, na ndio maana wakahamasishana kuanzisha ujenzi wa kituo hicho ili wawe salama na mali zao.

Kwa upande wake Katibu Msaidizi wa Umoja huo, Elisha Rugwisha, akisoma taarifa ya ujenzi huo wa kituo cha Polisi amesema ulianza Februari mwaka huu, na sasa upo katika hatua ya Renta, na unatarajiwa kukamilika mwezi huu kwa zaidi ya gharama ya Sh. Milioni 30.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza mara baada ya kumaliza kukagua ujenzi wa kituo cha Polisi kwenye machimbo ya madini ya dhahabu Mwakitolyo wilayani Shinyanga.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Shinyanga, John Kafumu, akizungumza mara baada ya kumaliza ukaguzi ujenzi wa kituo cha Polisi Mwakitolyo wilayani Shinyanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba, akizungumza kwenye ukaguzi huo wa ujenzi wa kituo cha Polisi katika Machimbo ya dhahabu Mwakitolyo wilayani Shinyanga.
Afisa kutoka TRA, Simon Mshofe, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TRA mkoani Shinyanga namna walivyoguswa na ujenzi wa kituo cha Polisi kwenye Machimbo hayo ya dhahabu Mwakitolyo, na kuamua kuunga mkono kwa kutoa Sh. Milioni 10.
Mwenyekiti wa wachimbaji wa madini ya Dhahabu Mwakitolyo, Aphonce Paulo, akizungumza namna waivyohamasika na kuanza ujenzi huo wa kituo cha Polisi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati) akikagua ujenzi wa kituo cha Polisi Mwakitolyo.
Ukaguzi ujenzi kituo cha Polisi Mwakitolyo ukiendelea.
Ukaguzi ujenzi kituo cha Polisi Mwakitolyo ukiendelea.
Ukaguzi ujenzi kituo cha Polisi Mwakitolyo ukiendelea.
Ukaguzi ujenzi kituo cha Polisi Mwakitolyo ukiendelea.
Ukaguzi ujenzi kituo cha Polisi Mwakitolyo ukiendelea.
Muonekano ujenzi kituo cha Polisi Mwakitolyo.

Post a Comment

0 Comments