Header Ads Widget

AHUENI KWA VYAMA VYA SIASA NCHINI YAJA, RAIS SAMIA KUKUTANA NA VIONGOZI WAKE


Na Damian Masyenene
IKIWA ni takribani miaka sita sasa baada ya zuio la mikutano ya vyama vya siasa nchini, huenda kukawa na ahueni kwa wanasiasa na vyama kuendesha mikutano yao na kupata uhuru wa kufanya shughuli zao mbalimbali.

Ahueni hiyo huenda ikawepo baada ya leo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutangaza kuwa anakusudia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini na  kuwasikiliza ili kulinda uhuru wa demokrasia kwa maslahi mapana ya taifa.

Baada ya kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais hayati Dk. John Magufuli, mikutano na shughuli mbalimbali za vyama vya siasa nchini vilizuiliwa kwa kile kinachoelezwa kuwa vinakwamisha na kurudisha nyuma kasi ya maendeleo.

Ambapo, inaelezwa kwamba kutokana na vitendo hasi vya wadau wa siasa na makundi ya wanasiasa wenyewe ambao baada ya kuingia kwa serikali ya awamu ya tano walianza kuchokonoa na hivyo kusababisha Rais kufikia uamuzi huo.

Akizungumza leo Aprili 22, 2021 jijini Dodoma wakati akilihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa licha ya kwamba Watanzania wanapaswa kuwa na uhuru wa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za kisiasa lakini wanapaswa kuzingatia na kuheshimu kanuni, miongozo na sheria mbalimbali za nchi.

"Ili kulinda uhuru wa demokrasia nakusudia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa Tanzania ili kwa pamoja tuweke mwelekeo wa kuendesha shughuli za siasa zenye tija na maslahi ya nchi yetu," amesema.

Kauli hiyo inakuja wakati viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakizuiwa kufanya mikutano pamoja na kushiriki katika mikutano tofauti ya kisiasa kama mahafali.

Wanasiasa na wanaharakati mbalimbali wa haki za binadamu nchini wamekuwa wakipinga kwa nguvu zote uzuiaji huo wa shughuli za kisiasa kwani ni kinyume cha Katiba ya Nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa, sheria namba 5 ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara.Post a Comment

0 Comments