Header Ads Widget

KATIBU MKUU AWATAKA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUWA WABUNIFU NA KULETA MATOKEO YA VIWANGO VYA JUU

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa Uongozi wa Kimkakati kwa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii, wakati wa Mkutano wa mwaka wa Wataalamu hao unaoendelea Jijini Ddoma.

Na Mwandishi wetu, Dodoma
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia mbinu na mkakati utakaowawezesha kufanikisha majukumu yao kwa viwango vya hali ya Juu.

Dkt. Jingu ameyasema hayo Jijini Dodoma leo alipokuwa anawasilisha mada kuhusu umuhimu wa Uongozi wa Kimkakati kwa wataalam wa maendeleo ya Jamii nchini CODEPATA wanapokuwa wakitekeleza majukumu.

Amewataka Wataalamu hao kuwa wabunifu na kuondokana na kufanya kazi kwa mazoea ili kuchochea mabadiliko katika Jamii zao na Taifa kwa ujumla.

“ Maafisa Maendeleo ambao ni viongozi, wanatakiwa kuwaza Zaidi, kuwa wabunifu na kufikiria namna bora ya kufanya mambo katika mwonekano tofauti na huo ndiyo Uongozi wa Kimkakati vinginevyo inakuwa kufanya kazi kwa mazoea,” alisema na kuongeza kuwa Uongozi wa kimkakati ni ule unaoleta mabadiliko katika nyanja husika.

“Afisa maendeleo ya jamii ni mtu wa kuchochea mabadiliko katika eneo alilopo na kama kiongozi wa Kimkakati lazima uwe na mambo kadhaa ikiwemo kuwa na dira au lengo mahususi, mahitaji ya kufikia lengo, Jinsi ya kufikia lengo na tathmini ya kina ya mazingira waliyopo”alifafanua Dkt. Jingu.

Jingu amesisitiza kuwa ili Maafisa hao waweze kufanikisha malengo husika kimkakati, ni lazima kujifunza nanmna ya kuwasilikiza walengwa, kujenga timu ya ushirikiano kiutendaji na kubwa zaidi ni kuzingatia misingi ya uadilifu ilivyo katika miongozo ya watumishi wa umma.

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wameomba Wizara kuendelea kuwajengea uwezo ili waweze kufanikisha majukumu yao.

Moses Kisibo amesema mikutano ya wataalam wa mandeleo ya Jamii ifanyike mara kwa mara kuanzia ngazi ya kanda na baadaye kupanda hadi kitaifa ili kujumuisha mawazo ya wanataaluma.

“Kuna wataalamu wengi lakini hawashiriki katika mikutano ya kujengeana uwezo wa kazi vinginevyo, Mkutano unaoratibiwa na CODEPATA unahusisha washiriki wenye uwezo wa kulipa ada na gharama nyingine,” alisema.

Kwa upande wake, Scholastica Gibore, wameiomba Wizara ya Afya, kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, kuwezesha Maafisa Maendeleo ya Jamii kupata mafunzo ya mara kwa ili waendane na kasi ya mabadiliko katika jamii. 

“Wengine tumehitimu miaka mingi iliyopita tukiendelea kutumia elimu hiyo katika kizazi hiki inakuwa ngumu na wakati mwingine tunaonekana kama viongozi wasio wa kimkakati,”alisema.

Mkutano Mkuu wa nne CODEPATA uliofunguliwa hapo jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima utafungwa tarehe 26 Februari, 2021.
Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu(hayupo pichani) wakati akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa Uongozi wa kimakakati katika utekelezaji wa majukumu yao.







Post a Comment

0 Comments