Header Ads Widget

USIMAMIZI SOKO LA MADINI DAR WAMKOSHA WAZIRI BITEKO, ATAKA LIWE KITOVU CHA BIASHARA

Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza wakati alipotembelea soko la madini la Dar es Salaam leo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameipongeza Tume ya Madini kwa kusimamia vizuri soko la Madini la jijini Dar es Salaam.

Waziri Biteko ametoa pongezi hizo leo Januari 11, 2021 kwenye ziara yake katika Soko la Madini la Dar es Salaam ambapo amekagua maduka ya wafanyabiashara wa madini pamoja na kuangalia namna mfumo mzima wa uuzaji wa madini unavyofanyika.

Katika ziara yake Waziri Biteko ameambatana na Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba na watendaji wengine kutoka Tume ya Madini.

"Nampongeza sana Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Maganga pamoja na timu yake; kiukweli mmenifurahisha kwa kufanya kazi kwa umakini mkubwa, taarifa zote zimewekwa kwa usahihi na hazina utofauti ambapo inaonesha upo umakini wa hali ya juu," amesema.

Ameongeza kuwa, kwa sasa Soko la Madini la Dar es Salaam ndilo Soko linaloongoza kwa kufanya biashara ya madini kwa umakini mkubwa na uaminifu na kuyataka masoko mengine kuendelea kuboresha utendaji kazi wake.

Ameendelea kusema kuwa Soko hilo limekuwa kituo cha kutegemewa kwa kuwa linaunganisha masoko mengine ya madini nchini na wafanyabiashara wa kimataifa.

"Natamani kuona Soko la Madini la Dar es Salaam linakuwa kitovu cha biashara ya madini nchini na kuaminika ndani na nje ya nchi," ameeleza.

Katika hatua nyingine Waziri Biteko amesema kuwa Wizara ya Madini inaangalia namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara ya masonara ikiwa ni pamoja na kuwahamishia kwenye Soko la Madini.

Aidha, Biteko amewakumbusha wafanyabiashara wa madini kufuata kanuni na taratibu za masoko ya madini ili kuleta tija.

Naye Afisa Madini mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Maganga amesema ofisi yake imeendelea kusimamia biashara ya madini kwa kuzingatia kanuni na taratibu za masoko ya madini

Wakizungumza katika nyakati tofauti wafanyabiashara wa madini wamepongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa masoko ya madini na kuwawezesha kupata faida kubwa zaidi.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa madini jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa TAMIDA, Othman Tharia amesema kuwa Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini wamekuwa mstari wa mbele kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa.

Amesema kuwa, Wizara ya Madini imeweka mazingira wezeshi kwenye masoko ya madini ikiwa ni pamoja na wataalam na vifaa vya kupima madini hivyo kurahisisha biashara ya madini.

Amewaomba masonara wote kufanya shughuli zao katika Soko la Madini ili kuwa na ulinzi wa uhakika wa mali zao na fedha huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.
Waziri Biteko akisisitiza jambo wakati akipitia taarifa mbalimbali za mauzo ya madini katika soko la madini la Dar es Salaam
Afisa Madini mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Maganga akizungumza katika kikao hicho

Wadau wa madini mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia kikao cha Waziri wa madini, Dotto Biteko alipotembelea soko la Madini la Dar es Salaam
Makamu Mwenyekiti wa TAMIDA, Othman Tharia akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa madini katika kikao na Waziri Biteko



Post a Comment

0 Comments