Header Ads Widget

MBUNGE KATAMBI AKAMILISHA ZIARA YA UJENZI VYUMBA VYA MADARASA JIMBONI, ACHANGIA SH MILIONI 34

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Patrobas Katambi (wa pili kushoto) akizungumza na viongozi mbalimbali alioambatana nao wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga wakati wa ziara yake ya ushiriki wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Kolandoto

Na Damian Masyenene, Shinyanga 
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Patobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) leo amehitimisha ziara yake ya siku mbili ya kushiriki shughuli za maendeleo kwa kutoa hamasa kwa wananchi juu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa jimboni kwake. 

Mbunge Katambi alianza ziara yake Desemba 31, mwaka jana kwa kutembelea kata 13 za jimbo hilo na kushiriki ujenzi katika shule zaidi ya 20, ambapo leo Januari 2, 2021 amehitimisha ziara hiyo kwa kuzitembelea kata za Kolandoto, Chibe, Old Shinyanga na Mwamalili. 

Katambi amezitembelea shule za sekondari Kolandoto na Mwangulumbi, huku za msingi akizifikia Mwalugoye, Old Shinyanga, Ng’wihandu, Mwamagulya, shule shikizi ya Ibadakuli, Twende Pamoja na kiwanda cha kufyatua tofali zinazotumika kwenye ujenzi huo kinachomilikiwa na Manispaa ya Shinyanga kilichopo kata ya Ngokolo. 

Katika ushiriki huo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa ikiwa ni mwitikio na utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa la kuhakikisha halmashauri zote zinakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi wasikose nafasi shule zitakapofunguliwa mapema mwaka huu, Naibu Waziri Katambi amechangia jumla ya Sh Milioni 34, ambapo ametoa Sh Milioni 1 kwa kila chumba kimoja cha darasa kinachojengwa. 

Akizungumza baada ya kuhitimisha shughuli zake leo, Mbunge Katambi ameeleza kuwa ushiriki wake katika shughuli za maendeleo ni mwanzo tu, kwani baada ya kukamilisha mahitaji katika sekta ya elimu yakiwemo madawati, vifaa vya maabara na walimu, kazi itahamia kwenye sekta nyingine ikiwemo afya, miundombinu, kilimo na biashara ili nazo zipewe msukumo huo na kuleta manufaa kwa wananchi. 

“Tumezunguka katika kata zote na kutembelea shule zaidi ya 24 na kote nilikopita nimechangia Sh milioni 1 kwa kila chumba cha darasa kinachojengwa, hivyo kufanya jumla ifike Sh Milioni 34 pamoja na kutoa motisha kwa mafundi na wasimamizi wa ujenzi huo. Nawashukuru viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla kwa kufanikisha hili na kujitolea nguvu na michango yao katika ujenzi huu,” amesema. 

Katika hatua nyingine, Katambi ameishauri halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuliangalia upya suala la mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu, kwa kubadilisha utaratibu na kujikita katika kuwawezesha kwa kununua vifaa zikiwemo mashine ili kuleta ufanisi badala ya kuwakabidhi fedha. 

“Sasa tujikite kwenye vifaa kwa kununua mashine na kuwawezesha kwani hili ni bora zaidi na uhalisia wake utaonekana na inakuwa endelevu hata kama mwanakikundi akikimbia vifaa vinabaki anakuja kujiunga mwingine,” amesisitiza. 

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila amesema kuwa ni ziara yenye mafanikio ambayo imeonyesha hali halisi ya namna wanavyotekeleza ujenzi wa vyumba vya madarasa katika manispaa yao, huku akieleza kuwa utekelezaji ni mzuri na kasi inaridhisha. 

“Tunataka idara zote zifuate kasi hii na kuiga utekelezaji huu, hatutakubali kufumbia macho kwa jambo lolote litakalotekelezwa kinyume na makubaliano na tunataka wote twende mguu sawa. Nitoe rai pale shule yetu mpya ya sekondari Mwangulumbi iliyopo kata ya Chibe usafi wa mazingira ufanyike ili itakapofunguliwa wanafunzi wasidhurike na mipaka ya shule pia iwekwe mapema,” amesema. 

Wakibainisha changamoto mbalimbali wakati wa ziara hiyo, Walimu wakuu wa shule, madiwani na watendaji wa kata wameeleza kukabiliwa na changamoto kubwa ya vyumba vya madarasa na kufanya baadhi ya madarasa kuwa na wanafunzi 240 ndani ya darasa moja, upungufu wa walimu, matundu ya vyoo na madawati. 

Moja ya shule zenye changamoto hizo ni ya Twende Pamoja iliyopo Kata ya Mwamalili ambayo ina wanafunzi 984 ikiwa na walimu wanne tu, ambapo Mtendaji wa kijiji, Edward Naholi ameiomba halmashauri kutatua changamoto kwani mwalimu mmoja hulazimika kufundisha wanafunzi 280, huku akieleza kuwa wanao upungufu wa walimu 26, matundu ya vyoo 26, madawati 6, nyumba za walimu 18 na madarasa 7. 

Nako katika shule ya msingi Ibadakuli yenye wanafunzi 1380 ikiwa na vyumba vinane tu vya madarasa na wanafunzi wa darasa la nne 218 wanaosomea chumba kimoja, kumekuwa na changamoto ya mlundikano wa wanafunzi darasani ambapo wamelazimika kuanza ujenzi wa shule shikizi ambapo wameanza na vyumba viwili na mpango wa baadae ni kuwa shule kamili na kujitegemea. 

Kwa upande wake, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Old Shinyanga, Judith Julius ameeleza kuwa shule hiyo inao jumla ya wanafunzi 1,374 wa awali na msingi na walimu 10 wakiwa na vyumba 12 tu vya madarasa, ambapo uhitaji ni vyumba 30 na pungufu ni 18, hivyo wameanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ambavyo vitagharimu Sh Milioni 13,003,000 hadi kukamilika kwake Januari 28, mwaka huu.
Mbunge Katambi akiendelea kuangalia maendeleo ua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Kolandoto
Jengo lenye vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Kolandoto ambao ni maalum kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa
Mbunge Katambi na viongozi wengine alioambatana nao katika ziara yake wakiwasili katika shule shikizi ya Ibadakuli kwa ajili ya kushiriki ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambapo alichangia Sh milioni 2 katika ujenzi huo
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi (kulia) akimuonyesha Mbunge Katambi ramani ya shule shikizi ya Ibadakuli ambayo baadae itajitegemea kutokana na iliyopo kwa sasa kuwa na wanafunzi wengi
Jengo lenye vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi shikizi Ibadakuli

Mbunge Katambi akipata maelezo ya namna kiwanda cha kufyatua tofali za kujengea vyumba vya madarasa kilichopo Kata ya Ngokolo kinachomilikiwa na halmashauri ya Shinyanga,kinavyofanya kazi. ambapo kiwanda hicho huzikopesha shule zinazojenga madarasa na kulipa baadae, huku kikifyatua tofali zenye ubora mkubwa na tofali moja likiuzwa kwa Sh 1,700
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila (katikati) akisisitiza jambo mbele ya Mbunge Katambi walipofika katika kiwanda cha kufyatulia tofali kinachomilikiwa na halmashauri hiyo kilichopo kata ya Ngokolo
Naibu Waziri, Patrobas Katambi pamoja na jopo lake wakiwasili katika shule mpya ya Sekondari Mwangulumbi iliyopo Kata ya Chibe inayotarajiwa kufunguliwa mwaka huu

Mh. Katambi akishiriki katika kufanya usafi wa mazingira kwenye shule mpya ya sekondari Mwangulumbi iliyopo kata ya Chibe, baada ya kufika shuleni hapo kushiriki na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa
Mbunge Katambi akiendelea na ukaguzi katika shule ya sekondari Mwangulumbi
Mbunge Patrobas Katambi (katikati) akizungumza baada ya kushiriki na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Mwangulumbi
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi akieleza maendeleo ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Mwangulumbi iliyopo kata ya Chibe inayotarajiwa kuanza masomo mwaka huu
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Old Shinyanga, Judith Julius akisoma taarifa mbele ya Mbunge Katambi, ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu unaoendelea shuleni hapo

Mbunge Patrobasi Katambi akishiriki kumwaga mchanga kwenye msingi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Old Shinyanga
Mbunge Katambi akishuhudia uchimbaji wa msingi wa chumba kimoja cha darasa katika shule ya msingi Twende Pamoja iliyopo Kata ya Mwamalili
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mwlaugoye iliyopo Kata ya Chibe, Peter Bangili akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya mandarasa shuleni hapo mbele ya Mbunge Patrobas Katambi
Mbunge Patrobas Katambi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga,Geofrey Mwangulumbi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar Gulam wakipata chakula cha mchana kwa mama ntilie katika soko la Nguzo Nane lililopo mjini Shinyanga.
Picha zote na Marco Maduhu

Post a Comment

0 Comments