Header Ads Widget

DK. JINGU AWATAKA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KURATIBU NGOs KIKAMILIFU

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt John Jingu wakati alipomtembelea ofisini kwake mjini Babati

Na Mwandishi wetu, Manyara
Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt John Jingu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) ili yafanye kazi kulingana na Sheria, Kanuni na taratibu za nchi. 

Dkt. Jingu ameyasema hayo mkoani Manyara wakati akifungua mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi wa Mashirika hayo kwa Mkoa wa Manyara kwa lengo la kuwajengea uwezo na uelewa wa namna bora ya kusajili na kuratibu NGOs

Amesema Maafisa Maendeleo ya Jamii, kisheria ni Wasajili wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wampewa jukumu hilo kwa mujibu wa matakwa ya sheria na kiutumishi.

"Tuzisimamie hizi NGOs zifanye kazi walizokusudia kufanya kwa mujibu wa Usajili wao hii itasaidia kutafuta changamoto zinazotukabilia katika kujiletea Maendeleo yetu" alisema.

Dkt. Jingu ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kutekeleza Miradi ya Maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kutatua changamoto na kuwaletea wananchi Maendeleo.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Manyara Said Mabie amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakizingatia kuwa majukumu walioyopewa Kisheria hivyo wayasimamie kwa uadilifu.

Naye Mwakilishi wa Msajili wa NGOs Mussa Leitura amewaasa Wasajili wasaidizi hao kufuata Sheria na Kanuni zilizopo ili kuhakikisha wanaondokana na changamoto za uwepo wa Mashirika katika maeneo yao unaleta mabadiliko na mchango katika maendeleo ya jamii.

Aidha Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Manyara Anna Fisso ameahidi kuwasimamia Wasajili wasaidizi katika Mkoa wake ili kuhakikisha Sheria taratibu na Kanuni za Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasio ya Kiserikali zinafuatwa kuhakikisha kunakuwa na Mashirika yenye tija kwa Taifa.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt John Jingu akizungumza na Wasajili Wasaidizi wa NGOs kutoka Halmashauri na Wilaya za Mkoa wa Manyara.

Afisa Ufuatiliaji na tathmini Mussa Leitura akieleza lengo la mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi wa NGOs Mkoa wa Manyara katika mafunzo kwa Wasajili wasaidizi yakiyofanyika Mkoani humo.
Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri za Mkoa wa Manyara na Wasajili wasaidizi wa NGOs wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kuhusu Usajili na uratibu wa NGOs

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW


Post a Comment

0 Comments