Header Ads Widget

TAKUKURU YAREJESHA SH. MILIONI 23.6 ZA WALIMU WASTAAFU KAHAMA, KAMPUNI ZA SUPER SALO, CLEOPHACE CREDIT ZAHUSIKA

Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kahama, Cosmas Shauri akimkabidhi fedha Sh. 15, 410,000 Paulina Malecha, fedha zilizookolewa kutoka kwa wakopeshaji wa mikopo umiza

Na Salvatory Ntandu -Kahama
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imefanikiwa kurejesha Shilingi Milioni 23, 610 ambayo ni mali ya Walimu wastaafu kutoka kwa wakopeshaji wa mikopo umiza na wadaiwa sugu wa Chama cha Walimu (CWT) Kahama Saccos Limited.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Desemba 2, 2020,  Kamanda wa Takukuru wa Wilaya hiyo, Cosmas Shauri amesema kuwa baada ya ofisi yake kupokea malalamiko kutoka kwa Walimu hao Wastaafu walianza uchunguzi haraka na kufanikiwa kuwakamata wahusika wote walikuwa wamekopa pamoja na kampuni zilizokuwa zinafanya biashara ya kukopesha fedha kwa riba kinyume cha sheria.

Amesema kuwa fedha hizo zimegawanyika katika Makundi mawili ambapo kundi la Kwanza jumla ya Shilingi milioni 15, 410,000 zinatoka katika Kampuni za Ukopeshaji za Mikopo umiza za Super Salo Limited na Cleophace Credit and Investment za Mjini kahama na Shilingi milioni 8 na laki 2 zimerejeshwa na wadaiwa sugu wa chama cha walimu Kahama Saccos Limited.

“Aprili 2019 Mwalimu Mstaafu Paulina Malecha alikopa shilingi milioni 3 kutoka kwa Kampuni ya Cleophace credit na kutakiwa kurejesha shilingi milioni 12 ifikapo June 2020 kwa riba ya shilingi milioni 9 sawa na asilimia 300 ya mkopo wake na hadi Takukuru tunapata taarifa alikuwa amekwisha kulipa Shilingi Milioni 9.

"Tulibaini pia kampuni ya Super Salo Investment ilimkopesha Mwalimu huyo tena Shilingi Milioni 4.8 na kumtaka kurejesha shilingi milioni 16 kabla ya June 20 mwaka huu kwa riba ya shilingi milioni 11 na laki 6 sawa na asilimia 241 kwa muda wa miezi 9,”amesema Shauri.

Amefafanua kuwa baada ya uchunguzi huo Takukuru iliziagiza kampuni hizo kutejesha fedha hizo haraka ambapo kampuni ya Cleophace Credit and Investment imerejesha Shilingi Milioni 5,650,000, huku Super Salo investiment wakirejesha shilingi milioni 9 laki 4 na elfu 60 mali ya Mwalimu Mstaafu Paulina Malecha.

“Shilingi Milioni 8,200,000 zimerejeshwa kutoka wa wadaiwa sugu wa chama cha Walimu Saccos ya Kahama ambapo wadaiwa hao walikwisha kutoroka baada ya kupata mikopo kutoka katika chama hicho na kusababisha baadhi ya walimu wastaafu kushindwa kupata stahiki zao,” amesema Shauri.

Kwa Upande wake, Mwalimu Paulina Malecha wakati akizungumza baada ya kukabidhiwa fedha zake ameishukuru taasisi hiyo kwa kumsaidia kupata haki zake kutoka kampuni hizo ambazo zilikuwa zinamdai riba kubwa ikilinganishwa na kiwango cha mkopo aliokopa kutoka kwa kampuni hizo.

“Nilikopa fedha hizo ili nigharamie Matibabu ya Mume wangu ambaye bado ni mgonjwa namshukuru Rais Magufuli kwa kutusimamia sisi wananchi wanyonge leo mimi nimepata haki yangu wapo watu wengi wanaendelea kunyanyaswa kutokana mikopo ambayo inariba kuwa hakika Takukuru mmenisaidia sana,” ameeleza.


Mkuu wa TAKUKURU Wilaya Kahama, Cosmas Shauri akimkabidhi fedha Sh 8,200,000 mwakilishi wa Walimu wastaafu, fedha hizo zimeokolewa kutoka kwa wadaiwa sugu wa chama hicho.
Hapa fedha zilizookolewa zikiwa mezani tayari kwa kugawanywa kwa walengwa.


Post a Comment

0 Comments