Header Ads Widget

MZEE WA MIAKA 75 AKAMATWA NA SILAHA 4 ZA SHOTGUN NA RISASI 36

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga Kamishina Msaidizi wa Polisi Debora Magiligimba akionesha Silaha zilizokamatwa na kwa Masanja Maziku Mkazi wa Kahama jana.

Na Salvatory Ntandu - Kahama
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Masanja Maziku Bugolole (75) Mkazi wa Kijiji cha Gula wilayani Kahama kwa tuhuma za kumiliki Silaha nne aina ya Shotgun, mitutu sita ya Shotgun na risasi 36 alizokuwa anazimiliki kinyume cha sheria.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana Desemba 17, 2020 mjini Kahama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba alisema kuwa Masanja alikamatwa Desemba 17 mwaka huu majira ya usiku nyumbani kwake kufuatia msako maalumu unaoendeshwa na jeshi hilo kwa lengo la kuwakamata wahalifu mbalimbali.

Alisema kuwa Silaha zilizokamatwa zimebainika kufutika namba zake za uhakiki na zingine zina namba lakini hazijasajiliwa kama sheria za umiliki wa silaha inavyoelekeza sambamba na kutokuwa na kibali cha kumiliki risasi 36 ambazo alikamatwa nazo.

“Silaha mmoja imebainika kuwa na uhakiki wa namba TZCAR 34951lakini usajili wake umefutika, silaha tatu hazina namba za uhakiki lakini zina namba za usajili ambazo ni Silaha namba D 172321,14999 na 24162,”alisema Magiligimba.

Kamanda Magiligimba alisema kuwa baada ya upelelezi wa ukikamilika Masanja atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Sambamba na hilo Kamanda Magiligimba alifafanua kuwa katika msako huo pia Jeshi hilo liliweza kuokota silaha mmoja aina ya Gobole katika kijiji cha Mpera wilayani humo ikiwa imetelekezwa kichakani na kuwataka wakazi wa mkoa wa shinyanga kutoa taarifa za watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.

TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807