Header Ads Widget

MR KUKU AHUKUMIWA KULIPA FIDIA YA ZAIDI YA BILIONI 5.4, FAINI YA MILIONI 5 AU KWENDA JELA MIAKA 5


 Picha ni jengo la Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam ambapo kesi ya Mr Kuku imeendeshwa 

 Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr. Kuku Farmer Ltd,  Tariq Machibya (29), maarufu kama Mr Kuku, aliyekuwa akikabiliwa  na kesi ya kufanya biashara haramu ya upatu  na kukusanya fedha za umma kiasi cha Shilingi  Bilioni 17, amehukumiwa kulipa fidia ya zaidi ya  Shilingi  Bilioni 5.4 baada ya kukiri Mashtaka ya kushiriki katika upatu na kupokea miamala ya fedha kutoka kwa umma.

Mahakama pia imemuhukumu mshtakiwa  kulipa faini ya shilingi  Milioni tano ama akishindwa atatumikia kifungo cha miaka mitano Gerezani.

Aidha Mahakama imeamuru fedha kiasi cha Shilingi Bilioni  5 na milioni 456 na laki 480.41 (5,456,480.41) ambazo zipo katika akaunti za mshtakiwa zitaifishwe na kuwa mali ya serikali. 

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Godfrey Isaya   amesema mahakama imezingatia kwamba mshtakiwa amekiri mwenyewe makosa yake na ni mkosaji wa mara ya kwanza na wameangalia makubaliano hivyo hakuna sababu ya kumpa adhabu kali.

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, wamedai mshitakiwa pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) wameingia makubaliano , katika mashtaka saba aliyokuwa anakabiliwa nayo yameondolewa na wamebakisha mashtaka mawili.

Akisomewa mashtaka hayo mawili, katika shtaka la kusimamia biashara ya upatu inadaiwa  kati ya Januari 2018 na Mei, mwaka huu, maeneo tofauti Jijini Dar ea Salaam alijihusisha na biashara hiyo kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma kwa kujifanya  watafanya ujasiriamali wa ufugaji kuku na watapata faida asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa uwekezaji wa miezi sita kiasi ambacho ni kikubwa kibiashara kuliko mtaji uliokusanywa.

katika shtaka la pili mshtakiwa anadaiwa kukubali kupokea muamala wa kifedha kutoka kwa umma kiasi cha Sh bilioni 17.

Awali mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka saba ambapo mbali na hayo mawili  yalikuwepo mashtaka matano ya utakatishaji  fedha.

Kabla ya kusomwa kwa adhabu, Wakili Kadushi aliieleza mahakama kuwa, hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya washitakiwa hivyo, ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria huku ikizingatia hatua ya makubaliano waliyofikia.

Upande wa wakili wa Utetezi, Augustine Shio ameiomba mahakama impunguzie mshtakiwa wake adhabu  kwani amekiri makosa yake mwenyewe na pia ana familia ya wake watatu ambao kila mmoja ana mtoto mchanga na wote wanamtegemea yeye.

Post a Comment

0 Comments