Header Ads Widget

WANANCHI WAHIMIZWA KUJENGA VYOO VYA KUDUMU KUEPUKA MAGONJWA YA MLIPUKO



Afisa Afya wa Mkoa wa Shinyanga, Neema Simba akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake

Na Suzy Luhende, Shinyanga
WANANCHI wa mkoa wa Shinyanga wameshauriwa kujenga vyoo bora vya kisasa katika msimu huu wa mvua, ili wasiendelee kujisaidia ovyo na kusababisha magonjwa mbalimbali ya mlipuko. 

Ushauri huo umetolewa na Afisa Afya wa Mkoa wa Shinyanga, Neema Simba, wakati akizungumza na Shinyanga Press Club Blog ofisini kwake jana, ambapo alisema watu wajenge vyoo bora vya kudumu ambavyo haviwezi kudondoka hata mvua zikiendelea kunyesha vitabaki kuwa imara, huku akisisitiza vyoo hivyo kufanyiwa usafi.

Neema amesema tayari wameshahamasisha katika wilaya zote za mkoa huo kupitia kampeni ya keujenga choo na matumizi ya vyoo bora, ambapo hatua zilizopigwa ni kubwa lakini changamoto imesalia kwenye matumizi na usafi wa vyoo hivyo.

"Unapojisaidia ovyo kinyesi hicho kinaponyeshewa na mvua maji hayo yanaelekea kwenye visima vya maji, ambapo wadudu wa kutoka kwenye kinyesi wanajikusanya humo unapokuja kuyatumia kama kuoga kunywa unaanza kuugua tumbo, watoto kupooza miguu, kina mama wajawazito wanaishiwa damu kutokana na minyoo inayotoka kwenye maji hayo kunyonya damu na minyoo hiyo hupasua utumbo wa mtoto na kusababisha kifo," alisema.

Alisema kabla hawajaanza kampeni ya kujenga vyoo bora watu wengi wakiwemo watoto walikuwa wanahatarisha maisha yao na wengine walikuwa wakipoteza maisha yao na kuanza kushikana uchawi na kusababisha migogoro kwenye jamii, bila kujua kwamba vinyesi wanavyojisaidia ovyo vichakani ndiyo vinasababisha kupoteza maisha ya watu wao.

"Ukiangalia katika familia wanaishi watu saba na wote hao wanajisaidia vichakani na ikinyesha mvua vinyesi hivyo vinasambaza maji kwenye visima, hivyo ni vizuri jamii ibadilike ijenge vyoo bora vya kudumu," alisema Neema.

Pia Neema alisema wananchi wanatakiwa kutengeneza vyoo bora na kuvifanyia usafi kwa kutumia maji safi na sabuni na kuendelea kunawa vizuri ili kuepukana na kupatwa na homa ya matumbo, pia ni vizuri watu watoke kwenye vyoo vya asili waende kwenye vyoo bora na jamii kujenga mazoea ya kuchemsha maji ya kunywa.


Alibainisha kuwa mkoa huo ulilenga kufikia asilimia 80 ya wananchi wake kuwa na vyoo bora kwa mwaka huu, lakini hadi kufikia April hadi Juni katika halmashauri zote za Shinyanga vyoo bora ni asilimia 60 ukijumlisha vyote na vya asili inakuwa ni asilimia 98.

Wakati wasio na vyoo ni asilimia mbili na uwepo wa vyombo vya kunawia mikono vyenye sabuni ni asilimia 32.3, vyoo ambavyo havina milango au paa la juu ni asilimia 38 na kaya ambazo zinatunza vyoo kwa usafi ni asilimia 26.5.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yudas Ndungile alisema wanaelimisha nyumba kwa nyumba wajenge vyoo bora ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko kwani gharama ni ndogo na kila mtu afanye hivyo kwa kujali afya yake.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Shinyanga akiwemo Charles Mahona na Magreth Ramadhan wamesema asilimia kubwa ya watu wamebadilika wamejenga vyoo bora lakini bado wachache wana vyoo vya asili na wengine hawajajenga kabisa mpaka sasa, hivyo ni vizuri wajenge ili watu wasiendelee kuugua matumbo.

Post a Comment

0 Comments